Kilio cha muda mrefu cha wanachama wa mfuko wa afya ya jamii
(CHF) hasa wale wa maeneo ya vijijini,mkoani hapa cha ufinyu wa wigo wa kupata
matibabu,sasa kimepata ufumbuzi wa kudumu.
Ufumbuzi huo unatokana na mfuko huo kufanyiwa maboresho
mbalimbali, ikiwemo kupata matibabu katika vituo vyote vya huduma za afya
mkoani hapa ikiwemo hospitali ya rufaa ya mkoa.Awali wanachama hao walikuwa
wakipata matibabu kwenye maeneo yao pekee.
Mkoa wa Singida,umechaguliwa kuwa mkoa wa majaribio ya
maboresho hayo,na halmashauri zake zimeagizwa kuwa hadi Februari, 10 mwaka huu,
ziwe zimeteua mameneja wa CHF ngazi ya halmashauri maafisa CHF ngazi ya tarafa na maafisa waandikishaji
katika vijiji.
Akizungumza kwenye kikao cha kazi cha kujadili utekelezaji
wa mfuko wa afya ya jamii ulioboreshwa, Mkuu wa mkoa wa Singida, Dk.Rehema
Nchimbi, alipongeza uamuzi huo wa serikali ambao umepanua wigo kwa wanachama
kupata matibabu ndani na nje ya makazi yao.
Akisisitiza, alisema kuwa wazo la kuufanyia maboresho mfuko
huo wa CHF,ni wazo chanya lenye tija na linalopaswa kuungwa mkono na viongozi
pamoja na watendaji wote.
Alisema kwa mujibu wa maboresho hayo,manachama wa CHF, sasa
anaweza kupata huduma ya matibabu hadi ngazi ya hospitali ya mkoa bila kikwazo
cho chote.
“Hili ni jambo jema sana.Mnatambua kwamba kilio hiki
kimekuwa cha siku nyingi hasa kwa
wananchi walioko katika maeneo ya vijijini, kwamba mfumo wa sasa hauwapi fursa
ya kuweza kupata matibabu bora pindi wanapokosa huduma pale walipo,” alisema.
Dk.Nchimbi alisema ili maboresho hayo yaweze kuwa na tija,
viongozi wanapaswa kutoa elimu kwa wananchi wauelewe mpango huo na nia ya
serikali ya kuboresha huduma za afya nchini.
“Mpango huu,ni lengo la serikali ya awamu ya tano katika
kuhakikisha kwamba kila mwananchi,anapata huduma bora ya afya zinazopatikana
kwa kutumia mifumo rasmi ya kuchangia kabla ya kuugua na kwa gharama nafuu.”
alisema.
Aidha, alisema ili wananchi wengi waweze kuvutiwa na mpango
huu huduma za afya vituoni na katika hospitali ya rufaa ya mkoa ni lazima
ziboreshwe kwa kiwango cha kukidhi mahitaji.
Pia mkuu huyo wa mkoa, ameagiza kwamba suala la bima ya afya
kwa wananchi wote, liwe ni agenda ya kudumu katika vikao vya maamuzi kuanzia ngazi
ya mkoa hadi ngazi ya kitongoji.
Awali Mkurugenzi wa CHF Taifa, Silvery Ngonza,alitaja baadhi
ya maboresho hayo kuwa kaya ya watu sita, italipa ada ya shilingi 30,000 ili
ipate huduma za matibabu kwa kipindi cha mwaka moja.
Alitaja maboresho mengine kuwa ni kuanzia sasa mkurugenzi wa
halmashauri atabaki na jukumu la kutoa huduma na kusimamia ubora.
“Mfuko wa taifa wa bima ya afya (NHIF), unabaki na jukumu la
kuwa mnunizi wa huduma. Kwa utaratibu huu,mkurugenzi wa halmashauri atatoa
huduma kwa wananchama na kisha kupeleka madai yake NHIF ili apate malipo.Huu ni
utaratibu unaotumika duniani kote,” alisema.
Kwa mujibu wa takwimu za hadi desemba mwaka jana (2016),mkoa
wa Singida ni wa kwanza nchini kwa usajili wa kaya katika mfuko wa afya ya
jamii (CHF).
Wilaya inayoongoza ni Iramba ikifuatiwa na Mkalama, Manyoni,
Simgida DC, Ikungi na Manispaa ya Singida.
No comments:
Post a Comment