
SIMBA SC leo imerudi kileleni mwa Ligi Kuu ya Vodcom
Tanzania Bara baada ya ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Prisons ya Mbeya, Uwanja
wa Taifa, Dar es Salaam.
Ushindi huo unaifanya Simba SC ifikishe pointi 51 baada ya
kucheza mechi 22, ikiwashushia nafasi ya pili mabingwa watetezi, Yanga SC wenye
pointi 49 za mechi 21.
Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Alex Mahaggi wa
Mwanza, aliyesaidiwa na Khalfan Sika na Abdallah Rashid wa Pwani, hadi
mapumziko Simba SC walikuwa mbele kwa mabao 2-0.
Mabao yote hayo yalifungwa na washambuliaji wazalendo, Juma
Luizio na Ibrahim Hajib na wote wakimalizia mipira kutoka pembezoni mwa Uwanja.
Alianza Luizio anayecheza kwa mkopo Msimbazi kutoka Zesco
United ya Zambia aliyefunga dakika ya 18 akimalizia krosi ya beki wa kulia,
Janvier Besala Bokungu kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kumchambua
kipa Aaron Kalambo.
Na Hajib naye akawainua vitini mashabiki wa Simba dakika ya
28 akimalizia pasi nzuri ya mshambuliaji Mrundi, Laudit Mavugo.
Simba ikajitahidi kupigania bao la tatu baada ya hapo,
lakini bahati mbaya kwao Prisons walikuwa wamekwishatulia na kuanza kudhibiti
hatari zote.
Kipindi cha pili nyota ya Simba SC iliendelea kung’ara na
wakafanikiwa kuunenepesha ushindi wao kwa bao la tatu lililofungwa na Laudit
Mavugo.
Mavugo aliye katika msimu wake wa kwanza Simba SC baada ya
kusajiliwa kutoka Vital’O ya kwao, Burundi alifunga bao hilo dakika ya 67 kwa
kichwa akimalizia krosi nzuri ya Ibrahim Hajib ambaye leo alikuwa katika
kiwango kizuri.

Winga Shizza Ramadhani Kichuya aliyetokea benchi kipindi cha
pili alikaribia kufunga dakika ya 81 kama si shuti lake kugonga mwamba na mpira
kurudi ndani na kumkuta Mavugo, ambaye alipopiga tena mpira ukaenda nje.
Nafasi nzuri zaidi Prisons walipata katika mchezo huo
ilikuwa ni dakika ya 12 baada ya Benjamin Asukile kuunganishia nje ya lango kwa
kichwa krosi ya kiungo Mohammed Samatta.
Baada ya mchezo wa leo, Simba wanakwenda kujichimbia
kujiandaa na mchezo dhidi ya mahasimu wao, Yanga Februari 25, Uwanja wa Taifa.
Kikosi cha Simba kilikuwa; Daniel Agyei, Janvier Bokongu,
Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Novaty Lufunga, Method Mwanjali/Mwinyi Kazimoto
dk62, James Kotei, Said Ndemla, Muzamil Yassin, Laudit Mavugo, Ibrahim
Hajib/Pastory Athanas dk74 na Juma Luizio/Shizza Kichuya dk70.
Prisons; Laurian Mpalile, Aaron Kalambo, Salum Kimenya,
James Mwasote, Nurdin Chona,
Jumanne Elfadhil, Lambert Sibiyanka, Kazungu
Nchinjayi/Kassim Hamisi dk38, Victor Hangaya/Salum Bosco dk76, Mohammed Samatta
na Benjamin Asukile/Meshack Suleiman dk56.
No comments:
Post a Comment