
Posho ya vikao ya mbunge wa Singida Magharibi Mh. Elibariki
Kingu, imetumika kuanzisha ujenzi wa zahanati nane katika jimbo hilo, ikiwa ni
njia ya kutekeleza uamuzi wake wa kutochukua posho hizo, na badala yake akitaka
ziwatumikie wananchi.
Mbunge huyo amebainisha hilo mapema wiki hii alipokuwa kweye
kipindi cha East Africa Breakfast, ambapo pamoja na mambo mengine alitakiwa
kueleza endapo anajua matumizi ya mgao wake wa posho za vikao vya Bunge, kwa
kuwa wakati Bunge la 11 likianza, alikuwa ni mmoja kati ya wabunge waliotangaza
kukataa kuchukua posho hizo.
Katika majibu yake Kingu alibainisha ilishindikana kuacha
kuchukua posho hizo kwa kuwa, kwa mujibu wa utaratibu wa Bunge, ni lazima
asaini kuzichukua, lakini akaamua kuwa yeye binafs asitumie hata shilingi, na
badala yake zikatatue kero ya zahanati jimboni kwake.

Mbali na zahanati, Kingu amesema pia kuwa kwa kutumia posho
hiyo, ameweza kuanzisha shule mpya za msingi katika maeneo mbalimbali ikiwemo
Winduwindu kata ya mwaru, Mtakuja kata ya Mwaru, Mtakuja kata ya Mtunduru,
Mwankalaja kata ya Mgungira, Mfumbuwahumba kata ya Ighombwe kata Minyughe na
Kinyarimi kata Minyughe.
No comments:
Post a Comment