NAIBU Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, `amemuumbua Naibu
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Dk. Hamis
Kigwangalla baada ya kukanusha taarifa ya bohari za dawa kuwa haziko chini ya
kiwango.
Naibu Spika huyo alilazimika kutoa maelekezo kwa serikali
kuangalia Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG)juu ya
ubovu wa bohari za dawa nchini na kuzifanyia kazi kasoro kama watazikuta.
Hatua hiyo ya Dk. Tulia ilitokana na Dk. Kigwangalla
kukanusha taarifa ya bohari za dawa kuwa chini ya kiwango zilizotolewa na
Mbunge wa Viti Maalum (CUF), Halima Ally Mohamed.
Mbunge huyo akiuliza swali la nyongeza, alisema kwa mujibu
wa taarifa ya CAG ya mwaka 2014/15, kuna bohari zisizo na viwango na kutaka
kujua msimamo wa serikali ili kuhakikisha afya za Watanzania.
Akijibu swali hilo, Dk. Kigwangalla alisema: “Kwanza, naomba
nikanushe vikali sana kwamba kuna bohari za dawa zisizo na viwango. Hiyo ni
ripoti ya CAG na hii ni taarifa ya serikali. Kwa hiyo naongea kama serikali kwa
mamlaka kamili niliyopewa.”
Alisema bohari zilizopo ni za viwango vya hali ya juu na
vimethibitishwa na Shirika la Kimataifa la Viwango (ISO), na zinakaguliwa kila
baada ya miaka mitano na dawa haziwezi kutunzwa kwenye bohari zisizo na viwango
kwa sababu zitaharibika.
“Dawa ni ‘high value items’ na hatuwezi kuzitunza ovyo,
hivyo kwa sababu tunazitunza kwa gharama kubwa na ndiyo maana katika utunzaji,
usambazaji mpaka katika kituo cha afya kijijini, kuna mnyororo uliokamilika
unaozingatia viwango vya ubora,” alisema Dk. Kigwangalla.
Kufuatia majibu hayo, Dk. Tulia alisema: “Mheshimiwa Naibu
Waziri, kwa kuwa mbunge ameuliza taarifa zinazotokana na Ripoti ya CAG,
serikali iangalie katika hiyo ripoti inasema nini ili kama alichosema mbunge
kipo sawasawa ama hakipo sawasawa.”
Alisema kama kinachosemwa kipo kwenye ripoti, Wizara ya Afya
iliangalie suala hilo.
Baada ya agizo hilo, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee, Watoto, Ummy Mwalimu, alisimama na kusema wamelipokea swali hilo
na watalifanyia kazi.
Katika swali la msingi, Mbunge wa Mpwapwa (CCM), George
Lubeleje, aliishauri serikali kuiwezesha Bohari ya Dawa nchini (MSD) kuwa na
fungu maalum kutoka Hazina.
Akijibu swali hilo, Dk. Kigwangalla alisema MSD haiwezi
kupewa fungu la moja kwa moja bila kupitia Wizara ya Afya.
No comments:
Post a Comment