WAKATI kikosi cha Simba, kesho Jumamosi kikitarajiwa kushuka
uwanjani kucheza dhidi ya Prisons ya Mbeya katika Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja
wa Taifa, Dar es Salaam, nahodha wa Simba, Jonas Mkude ametoa kauli kuhusu
nidhamu yake.
Mkude amesema kuwa yeye siyo mtovu wa nidhamu kama
anavyodaiwa kauli ambayo inaweza kupokelewa kwa hisia tofauti na wenzake na
mashabiki wa soka ambao mara kadhaa wamekuwa wakimlaumu kuwa ni mtovu wa
nidhamu.
Kauli hiyo imekuja baada ya taarifa kuwa kuna baadhi ya
wachezaji wenzake wa Simba wamemuomba kocha mkuu wa timu hiyo, Mcameroon,
Joseph Omog kumpokonya Mkude unahodha kutokana na nidhamu yake kuwa mbaya.
Mkude hakusafiri na timu yake kwenda Songea kucheza dhidi ya
Majimaji na inaelezwa kuwa wenzake hawakufurahishwa na kitendo hicho.
“Mimi siyo mtovu wa nidhamu kama inavyodaiwa na sijui ni kwa
nini nimekuwa nikiandamwa na tuhuma hizo kila wakati.
“Ninapokuwa sionekani katika timu siyo kwamba ninafanya
kusudi ila ninakuwa na matatizo na huwa natoa taarifa kwa viongozi wangu ambao
nawajibika kwao kila siku ambao ni kocha pamoja na meneja, lakini haya ambayo
yamekuwa yakisemwa kuwa sina nidhamu ninafanya mambo kwa kujiamulia siyo kweli.
“Kama kuna jambo lolote baya ambalo nililifanya na
halikuwapendeza na hiyo ndiyo ikawa sababu ya kusemwa vibaya kila simu basi
naomba wanisamehe,” alisema Mkude.
No comments:
Post a Comment