Kocha wa Singida United Fred Felix Minziro amesema sapoti
kubwa kutoka kwa mashabiki wa Singida ndio sababu pekee ya timu yao kupanda
daraja na kurejea ligi kuu Tanzania bara msimu ujao.
Kocha huyo wa zamani wa Yanga amesema, malengo waliyojiwekea
yametimia kwa kiasi kikubwa baada ya kufanikiwa kupanda kucheza VPL msimu ujao.
“Ushirikiano wa wachezaji, benchi la ufundi, viongozi na
mashabiki ambao wametupa sapoti kubwa kuhakikisha tunapata ushindi. Siri kubwa
ya ushindi wetu ni sapoti kubwa tuliyoipata kutoka kwa mashabiki wetu” – Fred
Felix Minziro.
“Malengo tuliyokuwa tumejipangia Singida United yametimia
katika kiwango kikubwa kwa maana kwamba tumeweza kuifunga timu ngumu kama
Alliance japo mechi ilikuwa ngumu.”
Mashabiki wengi waliingia uwanja wa Namfua mjini Singida
kushuhudia mchezo wa soka ligi daraja la kwanza kati ya Singida United dhidi ya
Alliance kutoka mkoani Mwanza mchezo ambao umeipa nafasi Singida United kurejea
ligi kuu Tanzania bara baada ya kusota kwa zaidi ya miaka 10.
Singida United ilipata ushindi wa magoli 2-0, mkongwe Nizar
Khalfan alianza kuifungia Singida bao la kuongoza dakika ya 14 baada ya mabeki
wa Alliance kuzembea kwa kudhani Nizar alikuwa ameotea.
Kipindi cha pili Singida United wakaandika bao la pili kwa
mkwaju wa penati uliopigwa Rashid Gumbo baada ya mchezaji wa Alliance kuunawa
mpira kwenye box.
Singida United sasa rasmi wamepanda daraja baada ya Rhino
Rangers ambao pia walikuwa na nafasi kulazimishwa sare huko mkoani Kilimanjaro
dhidi ya Panone na kuiacha Singida United ifikishe pointi 30 ambazo haziwezi
kufikiwa na timu yeyote ile kutoka kwenye kundi lao.
No comments:
Post a Comment