
MBUNGE wa Misungwi, Charles Kitwanga (CCM) ametishia kuwa
endapo wananchi wake hawatopata maji kutoka chanzo cha maji cha Ihelele kama
walivyoahidiwa na serikali, ataongozana na wananchi hao kwenda kuzima mitambo
ya maji katika eneo hilo.
Kwa mujibu wa mbunge huyo, chanzo hicho cha maji kwa sasa
kinazalisha maji yanayopelekwa katika maeneo mbalimbali ikiwemo Shinyanga na
Kahama kupitia Mamlaka ya Majisafi na Mazingira Kahama na Shinyanga
(Kashuwasa).
Akiuliza swali la nyongeza bungeni Dodoma mbunge huyo
alisema tangu serikali iwaahidi kuwa jimbo hilo la Misungwi litapata maji
kupitia mradi huo wa maji wa Ihelele hadi sasa maji hayo hayatoki wakati maeneo
mengine yanapata.
“Naibu Spika nasema wazi kuwa nitaongozana na wananchi wa
jimbo langu kwenda kuuzima ule mtambo wa maji Ihelele kama maji haya
yataendelea kutotoka kwenye maeneo yetu,” alisema Kitwanga ambaye aliposimama
kuuliza swali hilo alishangiliwa sana na wabunge wenzake.
Akijibu swali hilo, Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Gerson
Lwenge alimtaka mbunge huyo asiandamane na wananchi wake, kwani kilichokwamisha
maji hayo yasifike jimboni kwake ni uhaba wa fedha za kuunganisha bomba la maji
hadi eneo hilo ambapo zinahitajika takribani Sh bilioni nne.
No comments:
Post a Comment