Dar es Salaam. Rais John Magufuli amemteua Rogers Sianga
kuwa kamishna mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA).
Baada ya kuteuliwa Sianga alizungumza na Mwananchi na kusema
kwanza anamshukuru Mungu kwa uteuzi huo na akaahidi kushughulikia kwa karibu
kesi za vinara wa ‘unga’.
Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais
jana, Gerson Msigwa ilisema Sianga atasaidiwa na Mihayo Msikela atakayekuwa
Kamishna wa Operesheni na Fredrick Kibuta atakayekuwa Kamishna wa Intelijensia.
Uteuzi huo umekuja siku chache baada ya Mbunge wa Bunda
Mjini, Ester Bulaya (Chadema) kumtaka Rais Magufuli kuteua kamishna mkuu wa
tume hiyo, ambayo imekaa bila kiongozi tangu Sheria ya Kupambana na Kudhibiti
Dawa za Kulevya ilipotungwa mwaka 2015.
“Tusifanye siasa kwenye vita hii ya madawa ya kulevya,
tusimwongopee Rais kwa kutaka kuhakikisha vyeo vyetu tumwambie ukweli.
“Ili kumsaidia Rais anapaswa kumteua kamishina wa hii tume
maana tangu tulipopitisha sheria hiki chombo hakina kamishna, tutakapohakikisha
hicho chombo kinapata kamishna kwa kumsaidia Rais tutakamata wale wanaoingiza
dawa za kulevya, wale mapapa na si hao wanaokamatwa sasa hivi,” alisema
Bulaya.Mbali na Bulaya, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee alishauri bungeni kuwa
mapambano ya dawa za kulevya hayatafanikiwa bila kuiwezesha tume hiyo kifedha.
Sianga afunguka
Akizungumza na Mwananchi Sianga alisema kwanza anashukuru
Mungu kwa uteuzi huo, akaahidi kushughulikia kwa karibu kesi za vinara wa
‘unga’.
Kuhusu vigogo na wafanyabiashara maarufu walitajwa na Mkuu
wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, Sianga aliyekuwa Moshi mkoani
Kilimanjaro, alisema akifika Dar es Salaam atakutana na watendaji wengine
waangalie cha kufanya.
“Ndiyo kwanza nimeteuliwa bado nipo Moshi nikifika Dar es
Salaam, nitazungumza na wenzangu naamini tutashirikiana na tutashughulikia kwa
msingi wa sheria.
Pia, alitoa onyo kwa watu wanaolima mirungi au bangi nchini.
“Dawa hizo nyingine za kulevya ni ghali na zinaletwa kutoka
nje ya nchi, lakini mirungi na bangi tunajua inalimwa nchini hao wakulima
waache walime mazao ya vyakula, maana dawa hizo zinaleta madhara makubwa kwa
maendeleo ya taifa,” alisema.Uteuzi huo umekuja ikiwa pia ni siku chache baada
ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuanza kutangaza majina ya watu
anaotaka waripoti polisi kuhusiana na vita hiyo.
Huku kukiwa na maoni tofauti kuhusu hatua hiyo, Makonda
ameahidi kutangaza orodha nyingine ya tatu ikiwa ni sehemu ya mapambano yake ya
dawa za kulevya.
Washukiwa hao wamekuwa wakiripoti katika kituo kikuu cha
Polisi cha Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kwa ajili ya mahojiano kabla ya
kupelekwa mahakamani.
Mbali na uteuzi huo, Rais Magufuli pia amemteua Dk Anna
Makakala kuwa kamishna mkuu wa idara ya Uhamiaji.
Kabla ya uteuzi huo, Dk Makakala alikuwa mkuu wa chuo cha
Uhamiaji mkoani Kilimanjaro.
Taarifa hiyo imesema wateule hao wataapishwa kesho Ikulu ya
Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment