Watu 14 akiwemo Mchina, wanahofiwa kufa baada ya kufukiwa
katika mgodi wa dhahabu wa Kampuni ya RZ Union Mining Ltd uliopo Kata ya
Nyarugusu mkoani Geita.
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Ezekiel Kyunga jana alisema watu hao
wamefukiwa chini ya mgodi baada ya mlango wa kuingilia kwenye shimo la mgodi
kumeguka udongo na kujiziba.
“Usiku wa kuamkia leo (jana) saa tisa kwenye mgodi huo
unaoendeshwa na Wachina, mlango wa kuingilia mgodini mmoja ulimeguka na
kujifunga watu 14 wakiwa ndani,” alisema Kyunga.
Aidha, alisema mbali na watu hao 13, pia kuna Mtanzania
mmoja ambaye aliingia bila kujiandikisha na hiyo ni kwa mujibu wa watu
walioshuhudia tukio hilo hivyo kufanya idadi ya watu waliofukiwa kuwa 14.
Kyunga alisema tangu jana asubuhi jitihada mbalimbali za
kuondoa udongo kuwaokoa watu hao zinaendelea wakitumia mitambo na wataalamu.
“Kwa kusaidiana na Kampuni ya Geita Gold Mine (GGM) na
wataalamu wengine, jitihada zinaendelea ili kuhakikisha tunawaokoa watu hao,”
alisema Kyunga.
Alisema wakati huo huo wamefanikiwa kutoboa eneo jingine na
kupitisha mabomba ya hewa ya oksijeni ili kuwafanya watu hao wasikose hewa.
No comments:
Post a Comment