
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa
Njombe, Christopher Ole Sendeka kuchukua hatua kali kwa wote waliohusika na
upotevu zaidi ya shilingi bilioni moja za vyama vya ushirika.
Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo jana jioni (Ijumaa, Januari
27, 2017) alipozungumza na watumishi wa Mkoa wa Njombe wakati wa majumuisho ya
ziara yake ya kikazi ya siku saba mkoani hapa.
Alisema kati ya fedha hizo sh. milioni 532.736 zilipotea
katika SACCOS ya Kurugenzi Njombe pamoja na sh. milioni 900 zilizopotea katika
Chama cha Ushirika cha Akiba na Mikopo kiitwacho Wafanyabiashara Njombe SACCOS.
“Maofisa Ushirika nchini mmeendelea kudhoofisha jitihada za
Serikali katika kuimarisha ushirika. Katika eneo hili ninahitaji Mkuu wa Mkoa
ufuatilie suala hili na kuwachukulia hatua wahusiuka wote,” alisema.
Waziri Mkuu aliwaagiza Wakuu wote wa Wilaya kuwatumia
warajisi wa ushirika kuimarisha ushirika Mkoani Njombe.”Tunataka ushirika ulete
tija kwa wananchi na hatutaki ushirika ulioambatana na harakati za kugawa watu.
Endeleeni kuwashughulikia wanaushirika wasio waaminifu,”.
Aidha, Waziri Mkuu aliwasisitiza watumishi wa umma wote
nchini kuzingatia uadilifu, uaminifu, kutojihusisha na rushwa na kutumia
ipasavyo fedha za umma Serikali itachukulia hatua kali dhidi ya watumishi wote
wanaotumia nafasi zao kujinufaisha binafsi.
Alisema anataarifa za Watendaji wa Wakuu wa Wilaya ya Makete
akiwemo Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Bw. Francis Namsumbo, Mweka Hazina Bw.
Edward Mdagachule, Ofisa Utumishi, Bw. Nicodemas Tindwa na Mkaguzi wa Ndani Bw.
Michael Shija kuhusika na upotevu wa sh. milioni 71 zikiwemo sh milioni 41 za
UNICEF.
Waziri Mkuu alisema kuwa watumishi hao wamekuwa
wakijihusisha na vitendo vya utoaji wa rushwa kwa vyombo mbalimbali ili kuficha
ubadhilifu huo. “Mkuu wa Mkoa hakikisha hatua stahiki zinachukuliwa kuhusiana
na matukio haya,”.
Pia alimuagiza Mkuu huyo wa Mkoa kuhakikisha kuwa ……..wa
Wanging’ombe Bw. Edwin Kigoda anachukuliwa hatua stahiki kwa ubadhilifu wa sh.
milioni 37.9 zilizotolewa kwa ajili ya kuwajengea uwezo Walimu katika stadi za
Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK).
Mbali na watumishi hao pia Waziri Mkuu alimtaka Bw. Ole
Sendeka kumchunguza na kumchukulia hatua Ofisa Ardhi wa Mji wa Njombe, Bw. Addo
Kabange ambaye anatuhumiwa kuuza viwanja mara mbili, kuchukua rushwa na
kujipatia viwanja vingi kwa bei nafuu na kuviuza kwa wananchi kwa bei ya juu.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu alisema atawaelekeza Mkaguzi na
Mdhibiti Mkuu wa Fedha za Serikali (CAG), Msajili wa Hazina na Mrajisi wa
Ushirika kuanza kufuatilia malalamiko kuhusu umiliki wa kiwanda cha chai cha
Lupembe pamoja na kufuatilia mwenendo wa mgawanyo wa hisa za kiwanda hicho.
Alisema alipotembelea kiwanda cha chai cha Lupembe ambapo
alifarijika kukuta kiwanda hicho kimeanza kufanya kazi baada ya kusimama kwa
takriban miaka nane kutokana na mgogoro uliopo baina ya mwekezaji wa Kiwanda
hicho na Umoja wa Wakulima wa Chai Muvyulu.
Waziri Mkuu alisisitiza kwamba Serikali ya Awamu ya Tano
haitavumilia migogoro ya kuzuia ajira kwa wananchi, hivyo aliahidi
kushughulikia malalamiko kutoka pande hizo mbili na kutafuta njia ya kutatua
mgogoro uliopo.

Alisema baada ya kusomewa taarifa ya kiwanda na kwa upande
mwingine taarifa ya wanaushirika alibaini kuwepo kwa mgogoro unaohitaji
kutatuliwa ili kuwezesha shughuli za kiwanda kuendelea kwa amani na usalama.
Aidha, Waziri Mkuu alielekeza shughuli za ulimaji na uvunaji
wa majani ya chai kutoka kwa wakulima na kupeleka katika kiwanda hicho iendelee
na kiwanda kisisimamishe kazi ili kulinda soko la wakulima na ajira za
watumishi wa kiwanda hicho,” alisema.
Alisema kwa kuwa kiwanda hicho kinamilikiwa kwa ubia,
alimwelekeza Mkurugenzi wa kiwanda hicho kuhakikisha kuwa wanaweka wawakilishi
wawili au watatu wa wanaushirika katika Bodi ya Kiwanda hicho.
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu alizungumzia suala la
kuchelewa kuanza kwa mradi wa chuma cha Liganga, ambapo alisema ucheleweshaji
huo si wa makusudi bali ni mpango wa Serikali wa kujiridhisha na vipengele
mbalimbali vya mkataba ili uwe wa manufaa kwa Watanzania.
Hata hivyo, Waziri Mkuu alisema baada ya kutembelea eneo
ambalo uchimbaji utakapofanyika, na kujionea maendelezo ya wananchi yaliyopo,
alipata mashaka na kiasi cha sh. bilioni 13 kilichotengwa na wawekezaji kwa
ajili ya fidia kwa wananchi watakaopisha mradi huo.
Alisema Serikali haina budi kufanya tathmini ya kina na
kujiridhisha. “Nataka nimkumbushe Mheshimiwa Mbunge (Deo Ngalawa-Ludewa) na
Mwenyekiti wa NDC kujiridhisha na wahusika wanaotarajiwa kupata fidia hiyo,”.
Akizungumzia kuhusu maslahi ya watumishi, Waziri Mkuu
alisema Serikali kupitia Bodi ya Motisha na Mishahara inaendelea kufanya
tathmini ya uzito wa kazi ili kupanga upya viwango vya motisha na mshahara kwa
watumishi wote.
Pia aliwasisitiza waajiri wote wakiwemo Wakurugenzi kutenga
fedha kwa ajili ya likizo, masomo na uhamisho, kuandaa leave roster na mipango
ya mafunzo kwa watumishi.
IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAMOSI, JANUARI 28, 2017.
BY: BOAZ MWAKASEGE.
No comments:
Post a Comment