
Dar es Salaam. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imesema
haitaongeza siku za kufanya uhakiki wa namba ya utambulisho wa mlipakodi (TIN)
hapa jijini baada ya muda kumalizika leo, hivyo wote watakaokuwa hawajahakikiwa
watafutiwa namba zao na watatakiwa kuomba upya.
Kwa mara ya kwanza TRA imepanga kufanya uhakiki wa TIN kwa
siku 60 kati ya Agosti na Oktoba lakini baada ya kujitokeza watu wengi tarehe
ya mwisho iliongezwa hadi Novemba na mara ya tatu ilisogezwa hadi Januari 31.
Lengo la uhakiki huo ni kuondokana na mfumo wa kizamani wa usajili wa namba
hiyo.
Kayombo alisema kutokana na idadi kubwa ya watu waliokuwa
wanahitaji kuhakikiwa namba, mamlaka iliamua kusogeza mbele muda wa kutoa
huduma hiyo pamoja na kufungua vituo vya kutoa huduma ambako watumishi
walifanya kazi hiyo hadi Jumamosi na Jumapili kuwapa nafasi wafanyakazi.
Alisema madhara kwa watakaofutiwa TIN ni makubwa kwani
wafanyabiashara na madereva wa magari leseni zao zitakuwa batili na
watachukuliwa hatua kwa kosa la kufanya biashara bila kuwa na namba ya
utambulisho.
“Wale wote ambao watakuwa hawajahakikiwa watafutiwa namba
zao za TIN, itawalazimu kuomba upya ingawa kuomba kwao upya hakutafuta madeni
yao ya nyuma,” alisisitiza Kayombo.
Mmoja wa watu waliokwenda kuhakiki namba zao kituo cha
Mwenge, Abdul Namwelesi alikosoa utaratibu huo akipendekeza uhakiki ungekuwa
endelevu badala ya kuweka muda maalumu kutokana na ugumu wa watu wote
kuhakikiwa kwa wakati mmoja.
Alisema kutokana na ratiba ya maisha hususani kwa wakazi wa
Dar kuwa za kukimbizana, TRA wangeweka utaratibu maalumu kila dereva anapokwenda
kuhuisha leseni yake ahakikiwe taarifa zake
na kila mfanyabiashara anapokwenda kulipa kodi hapohapo ahakikiwe
taarifa zake.
Zulekha Kambi aliyekutwa kwenye kituo cha Uwanja wa Taifa
alijilaumu kutokana na kutotumia muda mrefu uliokuwa umetolewa badala yake
akasubiri hadi siku za mwisho zenye msongamano mkubwa.
“Najuta. Wee acha tu. Nilikuwa likizo nyumbani mwezi mzima.
Jana ndiyo nimekumbuka kesho mwisho. Nimekuja na nimekuta umati kama huu. Hapa
nilipo hata fomu sijui nitaipata saa ngapi,” alisikitika.
No comments:
Post a Comment