KOCHA Msaidizi wa timu ya soka ya Simba, Jackson Mayanja
amesema baada ya kutoka suluhu ya bila kufungana na Mtibwa Sugar katika mechi
ya Ligi Kuu juzi, nguvu zote sasa zinaelekezwa kuikabili Azam kwenye mchezo wao
wa Januari 28.
Mayanja, alisema hayo juzi baada ya kumalizika kwa mchezo
dhidi ya Mtibwa Sugar uliofanyika kwenye uwanja wa Jamhuri mjini hapa, ambapo
matokeo hayo ya sare ya bila kufungana yameifanya Simba iongoze ligi kwa
tofauti ya pointi mbili kutoka nne za awali.
“Mchezo haukuwa mbaya, wachezaji wamecheza vizuri, lakini
hawakuweza kupata magoli licha ya kupata nafasi zaidi ya mbili za kuwezesha
kupata ushindi,” alisema Mayanja.
“Tumemaliza mchezo wetu na Mtibwa Sugar na kuambulia pointi
moja, na sasa tunaelekeza nguvu kwenye mchezo wetu na Azam… huko tunajiandaa na
ushindi,” alisema Mayanja.
Mayanja alisema baada ya mchezo huo wanajipanga kufanya
mazoezi kwa ajili ya kukabiliana na Azam, na kutabiri kuwa mchezo huo utakuwa
mgumu kulingana na historia ilivyo kwa timu hizo kwa siku za hivi karibuni
zinapokutana.
“Siwezi kuizungumzia sana Azam kwavile mechi hiyo bado
lakini tunajipanga vizuri kuikabili kwenye mchezo huo,” alisema Mayanja.
Simba ilikutana na Azam kwenye fainali za Kombe la Mapinduzi
Zanzibar hivi karibuni na kulala kwa bao 1-0, matokeo yanayotabiri ugumu wa
mechi ya marudiano ya timu hizo. Katika mechi ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu
Simba ilishinda.
Aidha, Mayanja alisema kupata ushindi ugenini ni jambo gumu
na linachangiwa na sababu mbalimbali hivyo wanajiandaa kukabili michezo za
ugenini katika michezo ijayo. Pamoja na hayo, aliisifu Mtibwa Sugar kwa kucheza
vyema katika mchezo huo tofauti na iliyokuwa mchezo wao wa kwanza uliofanyika
Jijini Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment