TANGU vikatuni vya Hulk, jitu la kutisha na lenye nguvu
ijapokuwa la kufikirika vilipoanzishwa mapema katika miaka ya 1960, mashabiki
wamekuwa wakishangazwa na ushupavu au nguvu zaidi kuliko ghadhabu zake.
Tangu hapo kikatuni hiki kikapata nafasi katika tasnia ya
filamu, ambako alizidi kujipatia umaarufu miongoni mwa mashabiki kwa namna
alivyo.
Kuanzia hapo wale binadamu halisi wenye nguvu na maumbo
makubwa wakajipatia au kujipachika u-Hulk hususani nchini Marekani.
Katika Bara la Asia kulikuwa na Hulk wa Iran na sasa
amejitokeza Hulk wa Pakistan, ambaye ndiye makusudio ya makala haya.
Akiwa na uzito wa kilo 436, Arbab Khizer Hayat ameonesha
matendo mengi kama vile kusimamisha trekta kwa mikono mitupu.
Pia ana kundi kubwa la wafuasi katika mji wake wa nyumbani
wa Mardan, Pakistan.
Arbab Khizer Hayat, maarufu kama Hulk wa Pakistan mwenye
umri wa miaka 25 na urefu wa futi 6 na inchi 3 ana ndoto za kuiwakilisha
Pakistani katika mchezo wa mieleka wa uzito wa juu unaotambuliwa na Chama cha
Mchezo wa Mieleka Duniani (WWE).
Hayat ni mtu mwenye mwili mkubwa, anayehaha kuhakikisha
analinda umbo lake hilo la kutisha.
Mieleka na unyanyuzi wa vitu vizito ni mchezo unaopendwa na
wengi.
Hata hivyo, linapokuja suala la mtu kudai kuwa na nguvu
kuliko wote Pakistan huku akijiaminisha kuwa ni mwenye nguvu dunia bila
kuthibitisha hilo, kunashangaza wengi.
Hayat alianza kunenepa katika umri mdogo na akavutiwa na
mchezo wa mieleka na kunyanyua vitu vizito na hivyo kujiwa na ndoto ya kuwa mtu
mwenye nguvu duniani.
Nilianza kunenepa nikiwa mdogo lakini nilitambua kwamba
nahitaji kujiunga na mchezo wa kuinua vitu vizito na kuwa mtu mwenye nguvu
duniani. Hivyo, niliendelea kuongeza uzito,” Hayat anasema.
“Namshukuru Mungu kwa kunipa umbo hili. Haitachukua muda
kabla ya kuingia katika uwanja wa unyanyuaji vitu vizito duniani,” anasema.
Hayat, ambaye pia anajulikana kama Baba Khan, amejipatia
umaarufu katika mitandao ya jamii baada ya kuweka video zenye kuonesha nguvu
zake kwa kuzuia magari pasipo kutumia nguvu nyingi na au kuyainua kirahisi
rahisi.
Mnyanyua vitu vizito huyo hivi karibuni alidai kunyanya
kilogramu 5000 (tani 5) katika tukio lililofanyika nchini Japan mwaka 2012.
Anadai kutumia zaidi ya kalori 10,000 kwa siku ikiwamo mayai
36 kwa ajili ya kifungua kinywa, kuku wanne, kilo tatu za nyama nyekundu na
lita tano za maziwa.
Tajiri huyu kutoka Mardan amekuwa akitukuzwa katika mji wake
huo wa nyumbani.
Hata hivyo, watu wengi wanadai kwamba jitu hili linalofanana
na hulk ni feki.
Kuna watu wengi duniani wanasema kwamba madai ya Hulk huyu
wa Pakistan ni feki na kwamba uhalisia wa video zake unazua maswali mengi.
Video za Hayat, ambazo zinaonesha mtu huyo mzito akidhibiti
magari kwa kutumia nguvu kidogo huku magari yakijaribu kufurukuta kuchomoka
kutoka mikononi mwake bila mafanikio.
Lakini kiuhalisia nguvu kubwa inayotumiwa na magari hayo
ilipaswa kukata kamba, ambazo zilichomekwa tu, lakini hakuna kitu kama hicho
kinachoonekana kutokea.
Lingine linalozua maswali ni kwamba Hayat daima anaonekana
kuvaa nguo za kitamaduni za jamii ya Pathani nchini humo na kujifunika kwa
kashida (shali).
Hilo linampatia fursa ya kuuonesha mwili wake kuwa mnene mno
kuliko uhalisia.
Madai ya rekodi yake ya kunyanyua uzito wa kilogramu 5000
haijathibitishwa popote na imedaiwa ni uongo.
“Hakuna mtu anayeweza kuvunja rekodi hii,” alisema. Baba pia
alidai kwamba alipata medali kutoka WWE na jina lake liko katika Kitabu cha
Rekodi za Dunia (Guinness Book of World Records. Hata hivyo madai yake hayo
hayajathibitishwa.
Anasema kwamba hakuna utamaduni wa kunyanyua vitu vizito
Pakistan na hivyo yeye amelenga kubadili utamaduni huo.
Wakati Hayat anadai kuwa ni mtu mwenye nguvu kuliko wote
Pakistan pia anadai hana tatizo lolote la kiafya linalotokana na unene na uzito
wake huo mkubwa.
Hata hivyo, kwa kuzingatia masuala ya kiafya, mnyanyua vitu
vizito huyo anaweza asidumu katika ulingo wa WWE, ambako stamina ni muhimu
zaidi kuliko nguvu.
Chaguo la Hayat kuwa na uzito mkubwa wa kiasi hicho, kwa
mujibu ya wataalamu wa afya ni hatari na hauna afya, hata kama umelenga ubingwa
wa WWE au kuweka rekodi ya kuwa mtu mwenye nguvu kuliko wote duniani.
Kuna tofauti kati ya kuwa na uzito mkubwa na kuwa mwenye
nguvu na ni wazi jitu hilo la Pakistan liko mbali na ukweli.
No comments:
Post a Comment