Akiwa anajitayarisha kutoa album yake mwaka huu wa 2017, rapper Darassa hivi sasa ana uwezo wa kujiunga na wanamuziki wa kuimba wa Bongo Flava nguli Diamond Platnumz, Rais CEO wa kampuni ya muziki Africa WCB na hasimu wake wajadi kimuziki si mwingine bali ni Mfalme wa Bongo Flava Africa Alikiba, kwa kuwachuna Wakenya mamilioni ya pesa kwa hiyari yao kupitia ufanisi wake kimuziki na umaarufu unaozidi kupanda kila uchao hapa nchini Kenya.
Nikianzia na mjini Mombasa uswahilini hapa, nakupatia hali
halisi jinsi ilivyo. Nakutembeza katika mitaa kadha wa kadha ambapo mashabiki
wa muziki wa kizazi kipya wameupokea wimbo wa rapper Darassa ‘Muziki’ kwa
taadhima na heshima kubwa. Kuanzia kitongoji cha Lights, Soko Mjinga, Kisauni,
Mwandoni, Mtopanga, Bombolulu, Bamburi hadi kuvuka ng’ambo ya pili ya Ferry
Likoni mpaka Ukunda nyimbo, ‘Muziki’ inatamba kwa kasi zaidi ya mawimbi mazito
baharini.
Mbali na Pwani ya Kenya, sehemu za nyanda za juu na Ziwa
Victoria hadi Kisumu na Kenya yote kwa jumla. Kituo cha redio maarufu zaidi
nchini cha Citizen, kupitia kipindi cha Mambo Mseto kinachoendeshwa na
mtangazaji anayependwa sana na vijana Afrika Mashariki Mzazi Willy M Tuva, huwa
kipimo kamili cha ni mwanamuziki gani anayetamba kwa sana Afrika Mashariki
katika msimu fulani kwa kupitia requests zinazotumwa na mashabiki kwa kuitisha
nyimbo za wasanii wanaowakubali.
Msimu huu Darassa ameivunja rekodi kwa jinsi nyimbo yake ya
Muziki inavyoombwa kwa sana si radio Citizen pekee bali hadi vituo vingine
mbalimbali hata vile vinavyotangaza kwa lugha ya jamii fulani ama lugha ya mama
hapa Kenya.
Kimtazamo mji wa Mombasa ndio kitovu cha mafanikio kwa
wasanii wengi wa Bongo Flava kutamba nchi Kenya wanaobobea na waliobobea na
kufifia kimuziki. Nikiwataja baadhi tu wakiwemo Mr Nice ‘’Mzee wa Fagilia, Mr.
Blue jamaa la ‘Mapozi’, Ray C ‘Mrembo wa Wanifuatia nini’, Lady Jaydee ‘Dada wa
Siku hazigandi’, Proffessor Jay ‘Nguli wa Zali la Mentali’, Ferooz ‘Kigogo wa
Starehe.’ Alikiba, ‘Jamaa wa Cinderella’, Diamond Platnumz ‘Raisi wa Kamwambie’
Yamoto Band ‘Vijana wa Nitakupelepweta’ na wengine wengi.
Hii inapelekewa na sababu ya kuwa watu wanaoishi katika
pwani ya Kenya wengi wao hutumia Kiswahili na tokea jadi kabla ya muziki wa
kizazi kipya kuiteka nyara anga ya muziki wa pwani nchini Kenya wamekuwa
wakipenda sana muziki wa Taarabu ambao asili na chimbuko lake ni nchi ya
Tanzania hivyo wa pwani wanajua utamu wa Bongo Flava kabla kusambaa sehemu
zengine za nchi ya Kenya.
Makala ya: Changez Ndzai (Kenya)
No comments:
Post a Comment