
Wawanafunzi
wa Kidato cha Sita Shule ya Sekondari Usevya wilayani Mlele Mkoa wa Katavi,
wanadaiwa kuwashambulia kwa kuwacharaza viboko walimu wao wawili miongoni mwao
akiwemo Makamu Mkuu wa Shule hiyo, Makonda Ng’oka “Membele'‘ (34) ambaye
ameng’olewa meno matano kwa kipigo hicho.
Walimu hao
wawili wamedai kuwa hawako tayari kuendelea kufundisha katika shule hiyo huku
wakisisitiza kuwa ni fedheha kwao kucharazwa viboko na wanafunzi wao wenyewe
ambapo Mwalimu Gabriel Kambona aliachwa na ngeu kichwani.
Mei mwaka
huu, Ng’oka “Membele” alifikishwa katika Mahakama ya Mkoa wa Katavi kwa tuhuma
za kumlawiti mwanafunzi wake akidaiwa kutenda kosa hilo kati ya Novemba 2015 na
Aprili mwaka huu.
Ilisemekana
kukamatwa na kufikishwa mahakamani kwa Makamu Mkuu huyo wa shule hiyo
kulifuatia wanafunzi wa kiume wanaosoma Kidato cha Tano sasa wako Kidato cha
Sita katika shule hiyo kumkataa na kutishia kuandamana kupinga vitendo vyake
vya kuwalawiti wanafunzi wake.
Wanafunzi
hao walidai kuwa mwalimu huyo amekuwa akiwalawiti baadhi yao ikiwa ni adhabu
mbadala wanapobainika kufanya makosa shuleni hapo.
Hata hivyo,
baada ya kutopatikana ushahidi wa kumtia hatiani Ng’oka, Julai 27, mwaka huu
Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Wilaya ya Mpanda ilimwachia huru.
Mwalimu
Ng’oka aliripoti kwenye kituo chake cha kazi shuleni Usevya Agosti Mosi mwaka
huu ambako kurejea kwake shuleni hapo kunadaiwa kuamsha hasira kwa baadhi ya
wanafunzi wa Kidato cha Sita wakidai hawapo tayari kumwona mwalimu huyo na
familia yake shuleni hapo.
Akizungumza
na wanahabari jana mjini hapa, Ng’oka alidai kuwa hayuko tayari kuendelea
kufundisha kwenye shule hiyo akihofia usalama wake na kutokana na kipigo
alichokipata cha kushambuliwa na baadhi ya wanafunzi wake wa kidato cha tano na
cha sita wakati akiwa nyumbani kwake na familia yake.
Akisimulia mkasa huo, alisema Agosti 12, mwaka
huu usiku alikuwa nyumbani kwake shuleni hapo pamoja na familia yake pamoja na
mwalimu mwenzake, Gabriel Kambona aliyekuwa amemtembelea.
“Ghafla, saa
mbili usiku nikiwa maliwatoni nikioga lilitokea kundi la wanafunzi wa kidato
cha tano na sita wakiwa na silaha za jadi kama vile fimbo, marungu, mawe na
matofali na kuanza kuishambulia familia yangu pamoja na mwalimu Kambona,”
alieleza na kuongeza kuwa alilazimika ‘kuchomoka’ bafuni baada ya kusikia
mayowe yaliyokuwa yakipigwa na familia yake wakiomba msaada. Alipofika sebuleni
alishuhudia wanafunzi hao wakiishambulia familia yake kwa kuwacharaza viboko.
“Ndipo
walinigeukia na kuanza kunishambulia kwa kunipiga kwa marungu na fimbo hadi nikapoteza
fahamu nilizinduka nikiwa nimelazwa kwenye Kituo cha Afya Usevya na kubaini
kuwa nimepoteza meno yangu matano huku nikiwa nimejeruhiwa vibaya kichwani.
Baadaye nilihamishiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Mpanda ambako nililazwa
wiki moja na nusu kwa matibabu na sasa nimepewa rufaa niende Hospitali ya Taifa
Muhimbili jijini Dar kwa matibabu zaidi,” alieleza.

Alidai kuwa
uhasama baina yake na wanafunzi hao umedumu kwa muda mrefu, lakini anashangaa
uongozi wa Halmashauri ya Mpimbwe na Wilaya ya Mlele umeshindwa kumpangia kituo
kingine cha kazi na kuchukua hatua yoyote kwa wanafunzi hao licha ya kupeleka
majina yao kwa kuwa anawafahamu wote waliohusika.
Mwalimu
Kambona alidai kuwa hayuko tayari kuendelea kufundisha kwenye shule hiyo kwamba
kitendo cha kupigwa na wanafunzi wake kimemfedhehesha.
Kwa mujibu
wa mwalimu huyo, walimu wa shule hiyo waliketi baada ya kutokea kwa tukio hilo,
na walifikia maamuzi kuwa wanafunzi wote waliobainika kushiriki kuwashambulia
walimu wao wasimamishwe shule akidai kuwa uongozi wa Halmashauri ya Mpimbwe na
Wilaya ya Mlele ulipinga.
“Nimeandika
barua ya kuomba uhamisho kwani nia aibu kwangu kuendelea kufundisha wanafunzi
ambao wamenishambulia na kunitoa ngeo kichwani ….. siku hiyo ya tukio niliibiwa
simu mbili za kiganjani lakini jana nimefanikiwa kuikamata simu moja kwa
mwanafunzi wa kidato cha tano anayeitwa , Alex Maiko Makona na tayari
amemfikisha katika Kituo cha Polisi cha Usevya,” alidai.
Mwenyekiti
wa Chama cha Walimu (CWT) Mkoa wa Katavi, Gregori Mshota alisema tayari chama
chake kimeanza kuwasiliana na uongozi wa Halmashauri ya Mpimbwe na uongozi wa
Wilaya ya Mlele ili kuhakikisha mwalimu huyo anakuwa salama.
Ofisa Elimu
wa Mkoa wa Katavi, Ernest Hinju alidai kuwa suala hilo lipo ofisini kwake na
wameanza kulitafutia ufumbuzi. “Jambo hili linahitaji ushirikishwaji wa vyombo
mbalimbali ikiwemo Bodi ya Shule ya Sekondari ya Usevya,” alieleza.
Waziri Mkuu,
Kassim Majaliwa alipokuwa katika ziara mkoani Katavi mwezi uliopita, mke wa
mwalimu Ng’oka alitinga kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kijijini Maji
Moto akiwa na bango lenye malalamiko ya kutishiwa usalama wa maisha wa familia
yake, na Waziri Mkuu alimwagiza Kamanda wa Polisi wa Mkoa kushughulikia
malalamiko hayo.
No comments:
Post a Comment