VIFAA
vilivyokamatwa jana vya klabu ya usiku ya Bilicanas na ofisi ya gazeti la
Tanzania Daima, vyote vinavyomilikiwa na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, vitapigwa mnada na Shirika la Nyumba la
Taifa (NHC) siku 14 kuanzia jana, endapo atashindwa kulipa Sh. bilioni 1.2 za
deni la pango la miaka 20.
Mbowe
alikuwa mpangaji katika jengo la NHC lililopo makutano ya mitaa ya Mkwepu na
Indira Gandhi, katikati ya jiji la Dar es Salaam.
Vyombo hivyo
vilikamatwa jana na kampuni ya udalali ya Fosters Auctioneers and General
Traders iliyopewa kazi ya kuondoa vifaa hivyo baada ya Mbowe kushindwa kulipa
deni hilo ndani ya miezi miwili ya notisi ambayo shirika hilo lilikuwa
limempatia.
Meneja wa
Kitengo cha Kukusanya Madeni kutoka NHC, Japhet Mwanasenga aliyekuwa akisimamia
ukamataji wa vyombo hivyo, alisema Mbowe ana muda wa wiki mbili kuanzia jana
kulipa deni la Sh. bilioni 1.172 vinginevyo vitapigwa mnada.
Vifaa
vilivyokamatwa ni pamoja na kompyuta, meza na viti.
Alisema taratibu
zote zilifuatwa kabla ya kumuondoa mteja wao, ikiwamo notisi na kwamba vifaa
hivyo vitashikiliwa kwa muda huo wa wiki mbili.
“Tunashikilia
vyombo kwa muda wa wiki mbili na iwapo atashindwa kulipa vitapigwa mnada na
dalali, (mdaiwa) akishindwa kulipa anapangishwa mwingine,” alisema.
Alisema
shirika hilo linahitaji fedha kwa ajili ya ujenzi na uendelezaji wa majengo
yake hivyo mteja ambaye anadaiwa ajiandae kuondolewa wakati wowote na kwamba
zoezi la jana ni mwanzo tu.
Baadhi ya
watu wamelihusisha tukio la kuondolewa Mbowe katika ofisi hizo na masuala ya
kisiasa.
Lakini
Mwanasenga alisema uamuzi wa kumuondoa ofisi hizo hauna uhusiano na masuala ya
kisiasa.
Alisema
wapangaji wa jengo hilo wapo wengi pamoja na wadaiwa na kwamba baada ya
mchakato huo kuanza mdaiwa yeyote atakayeshindwa kulipa kodi ataondolewa.
Akizungumza
na waandishi wa habari katikati ya wiki iliyopita, Mkurugenzi Mkuu wa NHC,
Nehemia Mchechu alisema pamoja na Bilicanas, shirika linazidai taasisi za umma,
binafsi na watu binafsi jumla ya Sh. bilioni 15.
Notisi ya
siku 60 ya kuondoka Bilicanaa pamoja na majengo ya wadaiwa wengine
ilishatolewa, Mchechu alisema. Notisi hiyo ilikuwa inaisha juzi.
Alisema
baada ya muda huo kumalizika, utekelezaji wa kuondolewa katika majengo hayo
utaanza ukiambatana na uchukuaji wa hatua za kisheria.
Mchechu
alisema mbali ya Bilicanas, wadaiwa wengine ni Wizara ya Mawasiliano na
Uchukuzi inayodaiwa Sh. bilioni mbili, Benki ya Azania (Sh. milioni 161) na
Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa
(Sh. milioni 631).
Wadiawa
wengine walitajwa kuwa ni Wizara ya Afya na Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee
na Watoto (Sh. bilioni 1.3), Wizara ya Ujenzi (Sh. bilioni mbili), Tume ya
Utumishi (Sh. milioni 109) na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Sh.
bilioni moja.
Mchechu
alisema ukusanyaji wa madeni hayo kwa nguvu ni mkakati wa shirika hilo
kukusanya fedha ili kusaidia ujenzi wa nyumba za watumishi wanaohamia Dodoma.
"Mwaka
huu ujenzi unaanza Dodoma," alisema Mchechu, hivyo "fedha tunazodai
zitatusaidia kukamilisha uwekezaji mjini humo."
Alisema kuwa
fedha hizo zitatumika kwa ujenzi wa nyumba za watumishi 300 hadi 500 mkoani
Dodoma.
Alisema
ujenzi huo unatarajia kuanza mara moja na utachukua miezi 12.
Kwa mujibu
wa Mchechu, Sh. bilioni 60 za ujenzi wa nyumba hizo zitatokana na fedha za
ndani.
Alisema
shirika hilo limenunua ekari 240 eneo la Iyumbu, ekari saba Chamwino, nne Bahi
na Chemba ekari nne pia ikiwa ni kuunga mkono azma ya serikali ya awamu ya tano
kuhamia Dodoma.
Alisema
fedha nyingine zitapatikana baada ya nyumba 97 za shirika hilo zilizopo Medeli
mjini Dodoma kuuzwa.
No comments:
Post a Comment