
Raisi Dk.
John Magufuli ameshtukia mchezo unaofanywa na baadhi ya watu wakiwamo viongozi,
kuficha mabilioni ya fedha ndani na kutangaza uamuzi mzito wa kubadili noti
mpya ili wakose mahali pa kuzipeleka.
Kutokana na
hali hiyo, amewataka watu hao kuzitoa mara moja fedha walizoficha ndani ya
majumba yao chini ya magodoro ziingie katika mzunguko ili zikatumike kwenye
miradi ya maendeleo iliyopangwa kutekelezwa na Serikali ya awamu ya tano.
Kauli hiyo
aliitoa jana Dar es Salaam katika mkutano wa 14 wa mwaka wa wahandisi (ERB),
ambao uliwakutanisha wahandisi wa ndani na nje ya nchi ukiwa na lengo la
kujadili namna ya kuboresha mazingira ya kazi zao na kutafuta njia sahihi ya
kutatua changamoto zao.
Dk. Magufuli
alisema kuwa muda wowote anaweza akabadilisha fedha ili wanaozificha fedha hizo
za umma wapate hasara kwa kuwa wamesababisha hasara kubwa kwa wananchi.
Alisema
fedha nyingi zimepotea katika kulipa wafanyakazi hewa na kulipia miradi hewa
ambayo haitekelezeki na tayari ofisi yake imeanza kubaini na kuwafikisha
mahakamani, huku akiahidi hakuna mtu atakayeweza kuukwepa mkono wa sheria.
“Kuna mijitu
inaficha hela chini ya magodoro na mabenki, ninatamani kubadilisha fedha ili
wale wote walioficha ziwaozee huko huko. Katika siku hizi mbili ninaweza
kubadilisha fedha na waliozificha wazitoe wenyewe ili ziweze kuingia kwenye
mzunguko.
“Na
wajiandae hata siku hizi hizi mbili naweza kubadilisha fedha, hii meseji
iwafikie wale wanaoficha fedha kwenye magodoro na mabenki,” alisema Dk.
Magufuli.
Alisema
fedha za bure bure hazitakuwapo tena. “Kwa sasa watu watapata fedha kwa kufanya
kazi na huu ndio wakati wa kutajirika,”alisema Dk. Magufuli.
Akizungumzia
changamoto za sekta ya elimu nchini, alisema alipoahidi kutoa elimu bure
hakujua idadi ya wanafunzi ambao watapata elimu hiyo.
Alisema
katika kipindi cha nyuma walikuwa wanaandikisha wanafunzi wa darasa la kwanza
milioni moja na mwaka huu wameandikisha wanafunzi milioni mbili, hivyo ongezeko
hilo ni changamoto kwa Serikali yake.
“Shule za
sekondari wamefanikiwa kupata madawati kwa asilimia 98 na kwa shule za msingi
asilimia 88, zoezi la madawati tunakamilisha mwezi huu,” alisema.
Alisema hivi
sasa kuna wafanyakazi hewa na wanafunzi hewa. Kwa Mkoa wa Arusha wamebaini
wanafunzi hewa 10,000 na Mwanza 8,000.
“Idadi ya
wafanyakazi hewa hadi sasa wamefikia 16,500 kwa miaka yote, nawahakikishia bado
kuna wafanyakazi hewa, watafikia 20,500… hizo ndiyo changamoto kwangu,”
alisema.
Pamoja na
hali hiyo alisema kuwa mapato ya Serikali yameongezeka kutoka asilimia 26 hadi
40, na kwamba Septemba 19, wanatarajia kupokea ndege mbili aina ya Jet ambazo
zimelipiwa na fedha zilizobaki zipo tayari. Ndege hizo zitatua kwenye viwanja
vitatu.
UCHUNGUZI
VIWANJA VYA NDEGE
Dk. Magufuli
alisema katika bajeti ya mwaka wa fedha 2016/17, alitenga Sh bilioni 100 kwa
ajii ya kutengeneza na kukarabati viwanja vya ndege kwa kiwango cha lami.
“Uwanja wa
ndege Dodoma umegharimu shilingi bilioni 11. Kwa bajeti ya bilioni 100,
tulitegemea fedha hizo zitatengeneza viwanja vinane. Uwanja wa Mwanza
umegharimu shilingi bilioni 105 na upanuzi wa Uwanja wa Dar es Salaam shilingi
bilioni 600. Ni kwa nini viwanja viwili vimetumia gharama kubwa hivyo?” alihoji
Rais Magufuli.
Kutokana na
hali hiyo, alisema kuwa anataka kufanya uchunguzi ili kuweza kubaini ukubwa huo
wa gharama hali ya kuwa waliofanya tathmini ni watu anaowaamini.
Rais
Magufuli alisema hivi sasa kuna miradi mingi ya ndani ambayo inatarajiwa kuanza
ujenzi wake na kuagiza wapewe wakandarasi wa ndani ambao kama wataamua kufanya
kazi, ni wazi nchi itapiga hatua ikiwamo kufikia kuwa na taifa la uchumi wa
kati.
“Mchakato wa
kutengeneza reli ya kisasa ‘Standard Gauge’ tumetenga zaidi ya shilingi
trilioni moja na kuna kutengeneza bomba la mafuta kutoka Hoima hadi Tanga zaidi
ya kilometa 14,000. Je, wahandisi wa Tanzania tumejipanga vipi ili kuhakikisha
fedha zinabaki hapa?” alihoji.
USHAURI WA
WAHANDISI
Alisema hivi
sasa Serikali ipo mbioni kuleta ndege na meli ambazo zinahitaji wahandisi
ambapo alihoji ushauri wa wataalamu hao kuhusu vyombo hivyo.
“Wahandisi
tujitahidi kuzuia mchanga wetu. Katika vitu vinavyoniuma ni hicho, tumeibiwa
mno na tumechezewa mno, kila mahali ni dili, anachukua fedha anatumia anavyo
taka,” alisema.
Rais
Magufuli alisema Watanzania ni watu wa ajabu na wana kila kitu ikiwamo gesi
inayopatikana nchini.
“Nitashangaa
sana kwenye uongozi wangu wahandisi kama hamtasaidiana, na katika uteuzi wangu
nimependelea wahandisi na nimejitahidi kuwawekaweka kwenye kila eneo. Mnataka
nifanyeje wahandisi?” alisema na kuhoji.
Aliwataka
wahandisi hao wajitambue, wajipende na kwamba atafurahi siku moja ikiwa
wataweza kutengeneza kampuni yao.
“Mbadilike,
‘you need to change’, kila kitu kinahitaji mhandisi au aje malaika kutoka
mbinguni ndiyo mtabadilika? Muache wivu mtajenga nchi na msipoamua mtabaki kuwa
wasindikizaji,” alisema.
Awali akitoa
maelezo kwa Rais Magufuli, Mwenyekiti wa Bodi ya Wahandisi (ERB), Profesa
Ninatubu Lema, alisema hadi sasa idadi ya wahandisi 173,53 nchi nzima
wamesajiliwa. Wawili walikuwapo baada ya uhuru.
“Upungufu wa
fundi mchundo unasababishwa na kutokuwapo kwa mikopo katika vyuo wanavyosoma
katika ngazi ya stashahada na kukimbilia ngazi ya shahada kwa sababu wanapewa
mikopo ya kujikimu,” alisema Profesa Lema.
Mwenyekiti
huyo wa ERB, alimuomba Rais Magufuli aelekeze miradi yote mikubwa itumike kama
darasa la mafunzo kwa wahitimu.
Naye Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, alisema sekta ya
miundombinu ni muhimu katika kufanya maendeleo.
“Asilimia 59
ya barabara ni kiwango cha lami, lengo kubwa ni kuboresha usafiri wa maji na
nchi kavu,” alisema Profesa Mbarawa.
No comments:
Post a Comment