Avumaye
baharini papa…….., wakati Yanga ikionekana si lolote si chochote katika
mashindano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika, hapa nyumbani tunaamini Yanga
ndio timu bora kwa sababu ndio bingwa wa Tanzania na pia imeonesha ubabe kwa
timu nyingine za hapa nyumbani japo kwa upande wa kimataifa stori imekuwa
tofauti
Nimeanza na
mfano huu wa Yanga nikiifananisha na habari ya Timu ya Leicester City ya nchini
England. Mabingwa hao wa Ligi Kuu ya England walikuwa moto wa kuotea mbali
msimu ulioisha, wakizinyoosha timu kubwa za ligi hiyo na baadaye kuibuka
mabingwa.
Leicester
ndio mabingwa wa Ligi Kuu England na wataiwakilisha nchi katika mashindano
makubwa ya Uefa Champions League ikiwa ni mara yao ya kwanza tangu kuanzishwa
kwake. Katika mashindano hayo makubwa Leicester itakwaana na vigogo wa soka
barani Ulaya ambapo ili kufika mbali lazima wajifue kisawasawa.
Taswira
ilishaanza kujionyesha hasa katika mashindano ya International Champions Cup
yanayoendelea, Leicester City ilipokea kipigo cha mabao 4-0 toka kwa mabingwa
wa Ufaransa, Paris Saint-Germain wiki iliyopita na jana ikikubali kichapo tena
cha mabao 4-2 toka kwa mabingwa wa Spain Barcelona. Hii inaashiria nini?
Katika
michuano ya Uefa Champions League hakuna legelege, lazima timu husika
ijitathmini vilivyo, ukizingatia kule unakutana na vigogo ambao wana vikosi
bora, vilevile wana uzoefu mkubwa katika michuano hii. Timu kama Bayern
Munichen, Juventus, Real Madrid, Barcelona na nyinginezo huwezi kuzikwepa
kukutana nazo, iwapo unakubali kunyanyaswa na baadhi ya timu hizi unatarajia
nini katika mashindano?
Naiona
Leicester City ambayo haitaweza kutoa ushindani mkubwa katika mashindano ya
UCL, naamini watapambana kwa nguvu zao zote lakini kuna baadhi ya vigezo
wanakosa. Kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu England pekee haitoshi kukufanya mbabe
katika bara la Ulaya, hata Manchester City wana kikosi bora sana katika miaka
ya karibuni lakini hawajaweza kuonyesha maajabu zaidi katika mashindano ya UCL.
Vipigo
ilivyopokea Leicester City toka kwa PSG na BARCA ni fundisho tosha kwa timu hii
kujitathmini na kujitazama kabla ya kuanza kutupa karata yake ya kwanza kwenye
mashindano.
No comments:
Post a Comment