
Mwalimu wa
Shule ya Msingi Geitasamo iliyopo Kata ya Rung’abure wilayani Serengeti Mkoa wa
Mara, Raphael Charles (22) amenusurika kufa kwa kucharangwa mapanga kwa tuhuma
za kumpa ujauzito mwanafunzi wa kidato cha nne wa Shule ya Sekondari Ikorongo.
Mwenyekiti
wa Kijiji cha Geitasamo, Marwa Meng’anyi alisema mwalimu huyo amejeruhiwa kwa
kucharangwa mapanga na watu wanaodaiwa kuwa ni kaka wa mwanafunzi huyo baada ya
kuchukizwa na kitendo cha dada yao (jina linahifadhiwa) kukatishwa masomo kwa
kupata ujauzito.
Akizungumzia
tukio la kucharangwa mapanga, Mwalimu Charles alisema mkasa huo ulimkumba akiwa
njiani kwenda nyumbani akiwa ameongozana na mwalimu mwenzake aliyemtaja kwa
jina la Frank Batholomeo.
“Tukiwa njiani ghafla walijitokeza na kuanza
kunihoji kwa nini nimempa mimba mdogo wao, kabla sijajibu mmoja wao alichomoa
panga na kuanza kunishambulia akilenga kunikata shingo,” alidai Charles.
Alidai
katika jitihada za kujinusuru ilimbidi kutimua mbio, lakini alianguka chini na
vijana hao kufanikiwa kumfikia na kuendelea kumshambulia kwa mapanga.
Mwalimu huyo
aliyefungua kesi kuhusu shambulio hilo na kupewa namba ya jalada
Mug/RB/2886/2016 la kujeruhi, alidai alinusurika kuuawa baada ya mmoja wa
mafundi pikipiki waliokuwa eneo jirani kujitokeza kumsaidia.
Tukio la kushambuliwa
kwa mwalimu huyo limekuja huku madai dhidi yake kumpachika mimba mwanafunzi
huyo yakiwa yamefikishwa mahakamani kwa shauri namba 82/2016 tangu Mei 13.
Akizungumzia
kitendo chake na wanawe kumshambulia kwa mapanga mwalimu huyo, baba wa binti
aliyepachikwa mimba, Chacha Masiko alidai familia imechukizwa na kesi dhidi ya
mwalimu huyo kuahirishwa mara kwa mara bila wao kuelezwa sababu za msingi, huku
mshtakiwa huyo akiwatambia mtaani kuwa hatafungwa.
Mwalimu
aliyeshuhudia mwezake akicharangwa mapanga, Batholomeo alilaani kitendo cha
wanafamilia hao kujichukulia sheria mkononi na kuomba mamlaka husika kuchukua
hatua kukomesha vitendo hivyo vinavyoashiria uvunjifu wa amani.
Kaimu Ofisa
Elimu wa wilaya hiyo, Hawamu Tambwe alisema ameunda timu itakayoshirikiana na
uongozi wa kijiji kuelimisha wananchi umuhimu wa kuzingatia sheria katika
kushughulikia changamoto na matatizo yanayojitokeza kwenye jamii badala ya kuchukua
sheria mkononi.
Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Mara, Ramadhani Ngh’azi hakupatikana kuzungumzia tukio hilo
kutokana na simu yake kuita bila kupokewa, lakini mmoja wa maofisa wa polisi
wilayani hapa aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa jina alisema jeshi hilo
linawasaka ndugu hao ili wafikishwe mbele ya vyombo vya sheria.
No comments:
Post a Comment