
Licha ya
uongozi wa Chadema kutangaza kwamba umefuta mpango wa vijana wake (Bavicha), wa
kuisaidia polisi kuzuia mkutano mkuu wa CCM uliopangwa kufanyika mwishoni mwa
wiki ijayo, jeshi hilo limeimarisha ulinzi kila kona ya mji.
Mkutano huo
unaotarajiwa kufanyika Julai 23, utashuhudia Rais John Magufuli akipokea kijiti
cha uenyekiti wa chama hicho kutoka kwa mtangulizi wake Jakaya Kikwete.
Kabla ya
zuio la Mbowe, Bavicha walikuwa wameanza kujiandikisha katika maeneo mbalimbali
na kuchangisha fedha kupata nauli ya kuja mjini Dodoma kuzuia mkutano huo huku
polisi ikitangaza kupambana nao.
Jana, polisi
walifanya doria mji mzima wa Dodoma na kisha kukutana na wamiliki wa nyumba za
wageni na kuwataka wageni wote watakaofika kwenye nyumba hizo kusajiliwa kwa
vitambulisho vyao.
Tukio hilo
limekuja siku chache baada ya kukamatwa kwa viongozi wa Bavicha ambao jana
walifikishwa mbele ya Hakimu Mkazi Dodoma kusomewa mashtaka na baadaye kuachiwa
kwa dhamana wakidaiwa kukutwa na maandishi ya uchochezi kinyume na kifungu cha
32 (2) cha Sheria ya Magazeti, sura namba 229 iliyofanyiwa marekebisho mwaka
2002.
Waliofikishwa
mahakamani ni Mwenyekiti wa Taifa, Patrobas Katambi, Katibu Mkuu Julius Mwita,
Mwenyekiti wa Mkoa wa Mbeya, George Tito na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji,
Joseph Kasambala.
Akisoma
mashtaka yao mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, James Karayemaha,
Wakili wa Serikali, Lina Magoma alidai kuwa washtakiwa watatu; Katambi, Mwita
na Tito walikutwa katika Baa ya Capetown mjini hapa Julai 8 wakiwa na fulana
zilizoandikwa lugha ya uchochezi.
Alinukuu
maneno yaliyoandikwa katika fulana hizo kuwa ni “Mwalimu Nyerere: Demokrasia
inanyongwa na Dikteta Uchwara.”
Alisema
upelelezi unaendelea na kwamba hakuwa na pingamizi na dhamana. Kasambala
alifunguliwa jalada lake pekee licha ya shtaka lake kufanana na wenzake,
tofauti ikiwa mahali alipokamatiwa na ujumbe huo kwenye fulana aliyokuwa
ameivaa.
Wakili wa
Serikali, Beatrice Nsana, Kasambala alisema mshtakiwa huyo alikutwa katika
Kituo cha Polisi cha Kati Julai 9 akiwa amevaa fulana yenye maandishi; “Mwalimu
Nyerere: Demokrasia inanyongwa.” Washtakiwa wote walikana mashtaka yao na
Hakimu Mfawidhi Karayemaha, aliwapa dhamana baada ya kutimiza masharti na kesi
hiyo itatajwa tena Julai 26 mahakamani hapo.
Nje ya
Mahakama
Akizungumza
na wanahabari nje ya mahakama hiyo, Katambi alisema tangu walipokamatwa Ijumaa
iliyopita hawajawahi kuambiwa kosa lao.
“Tulipokuwa
Capetown tulipokwenda kula chakula walitokea askari waliovalia kiraia na
kutuvuta nje wakituambia mkuu wao anahitaji kuzungumza na sisi lakini cha ajabu
hawakutuambia kosa kwa muda wote tuliokaa ndani,” alisema.
Alidai kuwa
walihamishiwa katika rumande nyingine zilizopo Chamwino kutoka Kituo Kikuu cha
Polisi bila kuwaambia ndugu, viongozi wa chama chao wala mawakili wanaowatetea.
Alisema
katika rumande hizo kila mshtakiwa alifungwa kwenye chumba chake. “... Sisi si
majambazi lakini polisi wametumia nguvu kubwa kutukamata na kutushikilia bila
sababu ya msingi. Lakini tuna imani Mahakama itatenda haki katika shauri hili.”
Kuimarisha
ulinzi
Jana
asubuhi, polisi waliokuwa wamebeba silaha za moto, mabomu ya machozi na mbwa
walionekana wakizunguka kwa pikipiki na magari katika mitaa mbalimbali ya mji
wa Dodoma.
Msafara wa
magari zaidi ya 20 likiwamo basi kubwa lililobeba askari na gari la maji ya
kuwasha, lilizunguka katika mitaa mbalimbali kwa muda wa zaidi ya saa mbili.
Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa alisema mara nyingi wamekuwa wakifanya
mazoezi ya kutembea kwa miguu lakini wakati fulani huwa wanatumia vyombo
ambavyo wamepewa na Serikali kwa ajili ya kutekeleza majukumu yao.
“Leo
tumetoka kistaili ambayo pengine haijazoeleka. Hatukuwa na matembezi ya miguu,
tumetumia vyombo kwa maana ya pikipiki na magari yote tuliyonayo. Haya ni
mazoezi ya kawaida mara nyingi tunafanya doria,” alisema.
Alisema
doria hizo ni za pikipiki, miguu na magari na kwamba yote yaliyoonekana jana ni
katika kuwajenga askari kuwa tayari kwa ajili ya kukabiliana na lolote
litakalojitokeza akisema hayo ni mazoezi ya kawaida na kwamba waliojitokeza ni
maofisa wa polisi, wakaguzi, askari wa vyeo vya juu na vya chini.
Alisema
aghalabu wanafanya mazoezi hayo usiku lakini kwa jana waliona wayafanye asubuhi
ili kuwawezesha wakazi wa Dodoma kujivunia chombo chao cha polisi.
Alipoulizwa
kuhusu kauli za mitaani kuwa mazoezi hayo ni ishara kuwa wanaogopa vijana wa
Chadema, Mambosasa alisema polisi hawaogopi mtu yeyote.
“Kwanza
ijulikane tunafanya kazi kwa mujibu wa Katiba ya nchi, sheria, kanuni, mwongozo
na taratibu zote zinazoongoza nchi. Kwa hiyo tunachokifanya si mambo mapya ni
yale yaliyopo kisheria,” alisema.
Alisema
polisi hawaogopi wahalifu wa aina yoyote hata wa kutumia silaha na wamejipanga
kukabiliana nao.
“Na niwaambie
tu... haogopwi mtu hapa, sisi tunasimamia sheria kwa kuwaelimisha watii sheria
bila shuruti na wale wachache wasiotii tutawashurutisha,” alisema.
Alisema wale
wote wanaosema watafika Dodoma kulisaidia jeshi la polisi watawashurutisha kwa
kutumia nguvu kidogo tu ili warudi kwenye mstari.
No comments:
Post a Comment