Ukatili
uliofanywa na watu wasiojulikana wa kuwachinja watu wanane wa kitongoji cha
Kibatini mkoani Tanga, umesababisha wakazi wa kitongoji hicho kuanza kuyahama
makazi yao.
Watu hao
walichinjwa usiku wa Mei 31 nje ya nyumba ya mwenyekiti wa kitongoji hicho kwa
madai kuwa walisababisha “vijana” wao kukamatwa na polisi baada ya kutoa
taarifa zao wakati wakizurura kwenye eneo lao.
Waliouawa
katika tukio hilo ni mwenyekiti huyo, Issa Hussein, kaka yake, Mkola Hussein,
Hamis Issa, Issa Ramadhani na wengine wawili waliotambulika kwa jina moja la
Kadir, Mikidadi na Salum.
Jana baada
ya mazishi ya watu hao, mbunge wa Tanga Mjini, Mussa Mbarouk alipeleka lori
aina ya Mitsubishi Fusso kwa ajili ya kuwahamisha wanakijiji hao.
Wakazi
wayahama makazi
Diwani wa kata ya Mzizima, Fredrick Chiluba
alisema wakazi wa Kibatini wameamua kuhamia kitongoji cha Kona-Z kilichopo
kijiji jirani Kiomoni.
Mwandishi
alishuhudia wakazi takriban 60 wa Kibatini wakitoa vyombo, huku wengine
wakiezua mabati kwenye nyumba zao wakati wakisubiri gari ambalo baadaye
liliwasili na kuwachukua.
“Wameingiwa
na hofu ya kibinadamu na jambo hili lipo moyoni mwa mtu, hivyo huwezi
kumng’ang’aniza kukaa hapo wakati anahisi hayupo salama,” alisema Chiluba.
Hadija
Hussein alisema wameamua kuhama kwa sababu mara baada ya kukamilishwa kwa
shughuli za mazishi ya ndugu zao wanne, ilipofika saa 6:00 usiku, askari
waliokuwepo kwenye viwanja vya nyumba ya marehemu Mkola Hussein kulinda usalama
hawakuonekana.
“Tulipatwa
na wasiwasi mkubwa tulipoona askari na magari yao wameondoka, tukajua sasa na
sisi tunakuja kuchinjwa.Hatukupata usingizi kwa hofu, ndipo asubuhi tukaamua
kuondoa vyombo,” alisema.
Alisema
mbunge alipokwenda kuwahani, walimuomba gari la kuhamisha vyombo vyao ili
waondoke kabla jioni haijafika.
Mbunge
Mbarouk alisema alipowasili eneo hilo na kukuta hakuna ulinzi, alimpigia simu
mkuu wa polisi wa Wilaya ya Tanga ambaye alipeleka askari.
“Nilipowauliza
viongozi wa Jeshi la Polisi waliniambia askari wapo wanafanya kazi ya
kuzungukia maeneo, lakini haikuwa haki kuwaondoa askari mara tu baada ya
kufanyika mazishi,” alisema Mbarouk.
Mbunge huyo
alisema ameushauri uongozi wa polisi kupeleka ulinzi hata wanakohamia kwa
sababu wauaji lazima watapata taarifa ya waliko na wanaweza kuwatendea
chochote.
Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Tanga, Leonard Paulo alisema askari hawakuwa wameondoka kijijini
hapo bali walikuwa wamefanya mbinu za kufanya doria maeneo yanayozunguka
kitongoji hicho.
“Usiku huo
kwenye kitongoji kulikuwa na kikosi maalumu cha FFU ambacho mimi mwenyewe
nilikuwa nakiongoza usiku kucha. Tulikuwa tukifuatilia maficho ya wahalifu,
kitaalamu tunaita undercover,”alisema.
Kamanda huyo
alisema wakati polisi ikiendelea na operesheni, si vyema kuwatisha wananchi kwa
kuwa tangu yalipofanyika mauaji hayo, askari hawajaondoka.
RC: Mauaji
ya Tanga si ugaidi
Mkuu wa Mkoa
wa Tanga, Martine Shigela amesema mauaji yanayotokea katika mitaa ya jijini
Tanga na Amboni si vitendo vya kigaidi, bali yanatendwa na kundi la watu
wanaotaka kuvuruga amani.
Amesema hii
ni vita ya kiuchumi inahusiana na ujio wa bomba la mafuta ghafi kutoka Uganda
hadi Tanga na kwamba Serikali itahakikisha inawakamata waliohusika.
Alisema hayo
alipokuwa akizungumza na viongozi wa Serikali, Halmashauri ya Wilaya ya Muheza
pamoja na vyama vya siasa vya wa wilayani humo.
Shigela,
ambaye alikuwa katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Muheza kupokea taarifa ya
maendeleo ya kabla ya kuanza ziara wilayani humo, alisema Serikali haiwezi
kukubali kuona kundi la watu wachache wanaharibu amani iliyopo.
No comments:
Post a Comment