
Rais John
Magufuli amesema Serikali yake itaendelea kupambana na wanaoingiza bidhaa
zilizochini ya kiwango na wale wanaokwepa kodi.
Amesema kwa
kufanya hivyo, wanachangia kuviua viwanda vya ndani ya nchi.
Rais
Magufuli ameyasema hayo jana kwenye hafla ya utaoji wa Tuzo ya Rais ya
wazalishaji bora wa viwandani kwa mwaka 2015 zilizofanyika jijini Dar es
Salaam.
Tuzo hizo
zimeandaliwa na Shirika la Wenye Viwanda Nchini (CTI).
Rais amesema
pia hatawavumilia watendaji wote watakao wakwamisha wafanyabiashara wenye nia
ya kuanzisha viwanda nchini kwa sababu zisizo za msingi na kuwaahidi kuwasaidia
waweze kufanikisha ndoto zao.
Pia, amesema
ni vizuri wafanyabiashara wote nchini wakatumia fursa zipatikanazo katika awamu
hii ya uongozi wake, ili wasije kuzijutia baadaye.
“Nasema kwa
dhati kutoka moyoni, you have my support, mkishindwa katika kipindi cha awamu
ya tano basi hamtaweza tena,” alisema.
Rais
Magufuli alisema nchi inapokuwa na viwanda vingi vitatoa ajira kwa Watanzania,
vitaongeza mapato kwa Serikali na kuingiza fedha za kigeni kwa kuuza bidhaa nje
ya nchi.
“Nina
dhamira ya dhati ndani ya moyo wangu kuwasaidia wenye nia ya kuanzisha ya
viwanda, siwachukii matajiri nawapenda matajiri,” alisema.
Rais
Magufuli aliwapa moyo wafanyabiashara wenye viwanda kuanzisha vingine ili
Serikali iweze kunufaika zaidi.
Alisema
Tanzania ina rasilimali nyingi kama maliasili na madini na akawahakikishia
wawekezaji kuwa lipo soko kubwa la bidhaa watakazozitengeza lenye watu milioni
160 katika nchi za Afrika Mashariki na Kati.
Magufuli
alisema sekta ya viwanda ni muhimili mkubwa wa uchumi katika nchi huku akitolea
mfano wa nchi za China, India, Korea Kusini, Malaysia, Thailand na Vietnam ambazo zimekuwa kwa kasi kwa sababu ya uwepo
wa viwanda.
Alisema
viwanda vinapoanzishwa nchini badala ya kuuza mali ghafi kwa bei ndogo
zitatengenezwa bidhaa ambazo zitauzwa nje ya nchi na kutoa ajira kwa
Watanzania.
“Badala ya
kuuza ngozi tutengeneze viatu hapa hapa nchini au badala ya kuuza ng’ombe
Comoro tumepeke nyama iliyosindikwa,” alisema.
Alisema nchi
kama ya Sudan Kusini ina mahitaji makubwa ya unga wa mahindi.
“Lakini
wanaofaidika na soko hilo ni Wakenya ambao wanakuja nchini wananunua mahindi,
wanasaga na kuyapeleka huko,hivi wafanyabiashara tunashindwa hata kuanzisha
viwanda vya kusaga mahindi,” alisema
Alisema Mkoa
wa Arusha una ng’ombe wa maziwa lakini
yananunuliwa na Wakenya ambao wanayasindika kwenye viwanda vyao na kuja kuyauza
hapa nchini.
Hata hivyo,
alisema Serikali inaangalia uwezekano wa kuanzisha benki ya maendeleo ya
viwanda kwa lengo la kutoa mikopo yenye masharti nafuu na riba ndogo.
Kuhusu
kuondoa kwa changamoto mbalimbali zinazokwamisha maendeleo ya viwanda nchini,
Magufuli alisema Serikali imeshatenga Sh1trilioni katika mwaka wa fedha ujao
kwa ajili ya ujenzi wa reli ya kati kwa ajili ya kurahisisha usafirishaji wa
bidhaa mbalimbali.
Pia,
Serikali imeunda kamati maalumu itakayoangalia mazingira ya ufanyaji biashara
nchini ikiwamo kodi na tozo mbalimbali.
“Nchi yetu
inakuwa na kodi za ajabu ajabu, mfano zao la kahawa kulikua na zaidi ya kodi
30. Haya ndiyo tunayoyaangalia,” alisema.
Kuhusu upatikanaji wa mitaji na riba kubwa
zinazotozwa na benki, alisema katika kukabiliana na matatizo hayo Serikali
inajiandaa kuanzisha benki ya viwanda itakayowasaidia wenye wawekezaji.
Kwa upande
wake Waziri wa Viwanda, Biashara na
Uwekezaji, Charles Mwijage alisema Serikali imejikita katika kuhamasisha ujenzi
wa viwanda vingi zaidi nchini.
“Tumeandaa
mkakati wa pamba hadi inakuwa nguo, alizeti hadi mafuta na tunaendelea kufufua
viwanda vilivyokufa,” alisema.
Akizungumzia
changamoto zinazowakabiri wenye viwanda nchini, mwenyekiti wa Shirikisho la
Wenye Viwanda (CTI), Samuel Nyantahe alisema uchakavu wa miundombinu ya umeme
na miundombinu ya barabara imekuwa ikiongeza gharama za uzalishaji.
Pia,
alilalamikia uwapo wa utitiri wa kodi, mamlaka za usimamiaji biashara na uwapo
wa bidhaa bandia zinazotishia bidhaa za ndani
No comments:
Post a Comment