
Mahakama ya Rufaa nchini Kenya
imeamua viongozi wa chama cha wahudumu wa afya waliokuwa wamefungwa jela mwezi
mmoja waachiliwe huru mara moja.
Viongozi hao saba walifungwa
Jumatatu baada ya kupatikana na hatia ya kutofuata uamuzi wa ahakama wa
kumaliza mgomo wa madaktari ambao umedumu kwa miezi miwili unusu sasa.
Viongozi hao wametakiwa
kuhakikisha suluhu ya mgomo huo inapatikana katika kipindi cha siku saba.
Mazungumzo ya kutafuta suluhu
yataongozwa na Chama cha Wanasheria Kenya (LSK) na Tume ya Kitaifa ya Haki za
Kibinadamu (KNHCR).
Madaktari wamekuwa wakiitaka
serikali kuheshimu makubaliano ya mwaka 2013 ya kuwaongezea mishahara na
kuboresha mazingira ya utendaji kazi hospitalini Wanataka pia serikali iwekeze
zaidi katika dawa, vifaa na mitambo hospitalini pamoja na kutoa pesa zaidi za
kufadhili utafiti wa matibabu.
Wamekataa mshahara walioongezewa
na serikali wa asilimia 40 wakisema kuwa ni wa chini kuliko ule walioafikiana
mwaka 2013.
Karibu madaktari na wauguzi 5000
kutoka hospitali 2000 za umma, walianza mgomo wiki ya kwanza ya mwezi Desemba
na wagonjwa wamekuwa wakikosa matibabu.
No comments:
Post a Comment