
Hakuna kitu kibaya maishani kama kuonekana upo katika daraja
la chini na mtu wa kudharaulika kwenye jamii unayoishi. Kisaikolojia kuna
madhara makubwa.
Ni imani yangu kuwa kila mwanadamu timamu anapenda
kuheshimiwa lakini wengi wetu tunashindwa kupata heshima tunayoitaka kwa sababu
hatufahamu jinsi ya kuishi mbele ya wenzetu.
Kitaalamu, hakuna jambo ambalo hutokea maishani bila sababu
maalumu hivyo hata kudharauliwa kwako au kwetu ndani ya jamii tunayoishi
kunatokana na jinsi tunavyoenenda.
Njia za kukusaidia kurejesha heshima yako kwa kuperuzi na
wewe baadhi ya dokezo muhimu zinazoweza kukusaidia kujitambua na kuweza
kuyaepuka maisha ya kudharauliwa.
1. Muonekano.
Kwanza kabisa ni jinsi unavyoonekana. Muonekano
ninaouzungumzia hapa ni usafi wa mavazi na mwili kwa ujumla. Hata siku moja
hakuna mchafu anayeheshimika katika jamii anayoishi hata kama ana kipaji
kikubwa kiasi gani.
Kwa hiyo uchafu wa mavazi na mwili huchangia mtu
kudharauliwa katika jamii anayoishi.
Linaweza kuwa jambo dogo sana lakini ni moja kati ya sababu
kubwa inayochangia kuporomoka kwa thamani yako mbele ya wenzako.
2. Mazungumzo.
Hapa naomba nieleweke kuwa unachokizungumza kinaweza
kukujengea heshima au kukubomolea heshima. Kauli zisizo na busara zitakufanya
udharaulike kwa kila mtu. Uropokaji usiokuwa na mantiki huchangia kuporomosha
heshima yako hasa kama utakuwa muongeaji zaidi. Biblia inasema penye wingi wa
maneno hapakosi uovu.
3. Utendaji wako wa Kazi.
Ndugu zangu, siku zote heshima ya mtu ni kazi. Watu wengi
hawapendi kufanya kazi kwa bidii huku wengine wakijiendekeza kwa tabia ya
kuombaomba, jambo hilo halifai kwa vile huchangia kubomoa heshima yako mbele ya
jamii. Fanya kazi usiishi bila kujishughulisha.
4. Kutotimiza ahadi.
Kama una tabia za kuahidi mambo halafu unashindwa
kuyatekeleza, basi unajiweka katika nafasi mbaya ya kutunza heshima yako katika
jamii unayoishi. Bora ukwepe kutoa ahadi kuliko kuahidi na kutotimiza.

5. Sifa zisizo na maana.
Nakumbuka msemo mmoja kutoka kwa mwandishi mwandamizi
aliyekuwa mtaalamu wa falsafa za maisha, marehemu Adolf Balingilaki, ambao
unasema kwamba: “Ukitafuta heshima kwa gharama ya juu, basi utalipwa dharau kwa
bei nafuu.”
Msemo huu unamaanisha nini? Siku zote ukiwa unafanya mambo
yako kwa ajili ya kusifiwa au mazungumzo yako kuwa ya kujiinua, watu
watakudharau.
6. Kutokuwa mwaminifu.
Suala la uaminifu ni pana, kuna uaminifu wa fedha, siri,
dhamana na mambo kama hayo, hivyo ni vema kila unachoaminiwa lazima ukitunze
kwani ukiwa mtu wa kuvunja uaminifu fahamu kuwa utashusha heshima yako.
No comments:
Post a Comment