
Kondakta wa daladala linalofanya safari zake kati ya
Nguvumali hadi Raskozone, Salim Kassim amefariki dunia baada ya kudaiwa
kushambuliwa ndani ya kambi ya jeshi jijini hapa.
Kwa mujibu wa habari zilizopatikana na kuthibitishwa na
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga, Benedict Wakulyamba, kondakta huyo alikufa
wakati akipelekwa katika Hospitali ya Mkoa ya Bombo na chanzo cha kifo bado
kinachunguzwa.
Mwananchi ilielezwa kuwa tukio hilo lilitokea juzi usiku,
ambapo mashuhuda walidai kuona kondakta huyo akichukuliwa na wanajeshi na
kuingizwa kambini na baadaye alitolewa akiwa hajitambui
Akizungumzia tukio hilo, Khalid Juma mkazi wa Nguvumali
jijini hapa alisema askari hao wamekuwa na desturi ya kuwapiga wananchi bila
kuchukuliwa hatua zozote za kisheria.
“Tumekuwa tukipata vipigo kila wakati, licha ya viongozi
kupata taarifa za matukio hayo wamekaa kimya na hili tukio ni la tatu kutokea
hapa,” alidai Khalid.
Diwani wa Kata ya Nguvumali ambaye pia ni Meya wa Jiji la
Tanga, Alhaji Mustapha Selebosi alisema sababu za kipigo hicho ni mwanafunzi wa
shule moja jijini Tanga ambaye ni mtoto wa ofisa wa JWTZ kuzozana na kondakta.
KUTOKA: GLOBAL PUBLISHERS
No comments:
Post a Comment