
KABLA ya mwanzoni mwa Machi, 2013 mwanadada mwenye asili ya
Kenya na muigizaji mahiri duniani, Lupita Nyongo hajatangazwa na mchekeshaji
Will Smith mjini Los Angeles, Marekani kuwa ndiye mshindi wa Tuzo ya Oscar
kupitia kwenye filamu yenye maudhui ya utumwa iitwayo 12 Years A Slave, iko
wazi ni watu wachache waliokuwa wanamfuatilia duniani.
Huo ndiyo ukweli halisi maana hata vyombo vya habari
vimeanza kumuandika zaidi baada ya tuzo hiyo. Hata hivyo kiuhalisia si kwamba
filamu hiyo iliyompa tuzo akiwa Muigizaji Bora Msaidizi wa Kike ndiyo ya kwanza
kwake kufanya.
Ameonekana kwenye filamu nyingi na michezo ya jukwaani
mbalimbali ikiwemo The Winter’s Tale, Lights, Chekhov’s Uncle Vanya na The
Taming Of The Shrew ulioandaliwa na mwandishi maarufu duniani William
Shakespeare.
Hata hivyo mbali na michezo hiyo pia Lupita Nyongo alitikisa
kwenye tamthilia ya MTV iitwayo MTV Shuga kwenye msimu wa kwanza, tamthilia
ambayo mwanadada kutoka Bongo, ambaye ni mwanamuziki mwenye ‘fun base’ kubwa
Afrika kwa sasa, Vannesa Mdee ‘Vee Money’ au
Cash Madame amepata shavu la kuuza sura katika msimu wa tano. Jambo
linalokamilisha usemi kuwa anapasua mulemule alimopita Lupita Nyongo.


Showbiz: Katika makala hii, Vee Money akifanya mahojiano na
Uwazi Showbiz, anaelezea kwa upana ‘career’ yake hiyo mpyaUmepata shavu la
kuuza sura kwenye tamthilia, hebu elezea kinagaubaga, tamthilia inaitwaje na
ilikuwaje ukapata mchongo huo?
Vee Money: Ni Tamthilia ya MTV inaitwa MTV Shuga. Huu ni
msimu wao wa 5. Nilipata kazi kwa kufanya ‘audition’ baada ya wao wenyewe
kuniomba nifanye hivyo.
Showbiz: Baada ya kupita kwenye audition, ni ugumu gani
umekutana nao lokesheni na ni tofauti kabisa na kushuti video za muziki?
Vee Money: Hakuna ugumu wowote labda tu kumeza script. Ni
kazi ngumu lakini kwa kuwa nimeamua kufanya, inabidi kukomaa.
Showbiz: Vipi kuhusu nafasi uliyopewa kucheza, imeendana na
wewe na umeifurahia?
Vee Money: Kiukweli kwenye ‘character’ pia kulikuwa na
changamoto kwa sababu aina ya mwanadada niliyetakiwa kucheza, siendani naye
kabisa, lakini kwa kuwa ni kazi ya sanaa haikuwa na budi kufanya kila
nililotakiwa kufanya ilimradi tu kuitendea haki nafasi hiyo.


Showbiz: Tamthilia hii inafanyikia wapi?
Vee Money: Johannesburg, South Africa
Showbiz: Unatumia muda gani kukaa lokesheni?
Vee Money: Nakaa siku kumi lokesheni. Lakini pia kila baada
ya wiki mbili ninakuwa naenda maana tamthilia yenyewe itatoka April.
Showbiz: Umegundua nini tofauti kati ya uandaaji wa filamu
na tamthilia za Kibongo na nje?
Vee Money: Sijawahi kushiriki kutengeneza filamu za
nyumbani, kwa hiyo sifahamu lolote, lakini wenzetu nje wanajipanga sana.
Showbiz: Ni waigizaji gani wengine maarufu ambao umeigiza
nao?
Vee Money: Wapo wengi, kutoka Afrika Kusini na Nigeria,
siwezi ila kuwataja kwa majina.
Showbiz: Kuhusu malipo vipi, unaweza kuzungumzia lolote?
Vee Money: Kikubwa ni kwamba kila ninapokwenda wananiita
Cash Madame, so hata kama ni malipo ni ya kuridhisha tu.
Showbiz: Kabla ya
kupata nafasi hii, uliwahi kuwaza siku moja kuwa utakuwa muigizaji?
Vee Money: Ndiyo, ni ndoto zangu za muda mrefu sana, so
namshukuru Mungu amenionyesha mlango nategemea kufanya zaidi ya hiki
ninachokifanya.
Showbiz: Ni muigizaji gani unamkubali zaidi duniani?
Vee Money: Viola Davis
Showbiz: Nini mipango yako zaidi kuhusu muvi na tamthilia?
Vee Money: Nitaweka wazi wakati ukifika.
Showbiz: Kipi ambacho unapenda Watanzania wakifahamu ambacho
sijakuuliza.
Vee Money: Hii tamthilia ndiyo ilimtoa Lupita Nyongo,
aliigiza kwenye msimu wa kwanza, kwa hiyo mimi pia wategemee mambo makubwa
sana.
Showbiz: Nakushukuru kwa ushirikiano Cash Madame na kila la
kheli katika ‘keria’ yako.
Vee Money: Asante
No comments:
Post a Comment