
MWENYEKITI wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki (EAC), Rais
John Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Mke wa Mwanzilishi wa Taifa la
Sudan Kusini, Rebecca Nyandeng Garang de Mabior, Ikulu jijini Dar es Salaam
jana.
Baada ya mazungumzo hayo, mke huyo wa Mwanzilishi wa Taifa
la Sudan Kusini, Rebecca Mabior alisema yeye na ujumbe wake wamelazimika kufika
nchini Tanzania kuonana na Dk Magufuli ambaye ni Mwenyekiti wa EAC kwa lengo la
kumfahamisha hali halisi ya nchi ya Sudan Kusini, huku wakimuomba ashirikiane
na viongozi wenzake wa EAC kuisaidia Sudan Kusini kutafuta suluhisho la mgogoro
unaolikabili taifa hilo.

“Tumefarijika kuwa hapa katika Ikulu ya Tanzania na tuko
hapa kumsihi Rais Dk Magufuli kama Mwenyekiti wa jumuia ya Afrika ya Mashariki
akishirikiana na viongozi wenzake wa jumuia hiyo kuona namna gani wanaweza
kutusaidia ili Taifa la Sudan Kusini liwe Taifa lenye amani.
“Hivyo hapa tunawakilisha vilio vya watu wa nchi yetu na
kikubwa tunachokitaka ni Amani katika nchi yetu na hiki ndio kilio chetu,”
alisema Mama Rebbeca Mabior.
Naye Rais Magufuli amewasihi viongozi na wananchi wa Sudan
Kusini kutafuta njia mwafaka ya kumaliza tofauti zao kwa njia ya amani na ili
kuepuka machafuko yanayosababisha mateso kwa wananchi wa Taifa hilo.
“Mama Rebecca hata mimi binafsi naumizwa na kile
kinachoendelea katika nchi ya Sudan Kusini hivyo, ningezisihi pande zote zinazotofautiana
kumaliza tofauti zao kwa amani kwa mustakabali wa maendeleo ya Taifa la Sudan
Kusini,” alieleza Rais Magufuli kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu.
Chanzo: MTEMBEZI.COM
No comments:
Post a Comment