BARAZA Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) limesikitishwa na tabia
iliyoanza kujengeka ya kuihusisha Dini ya Kiislamu na vitendo
vinavyoashira ugaidi vilivyojitokeza nchini katika siku za hivi karibuni
na kugharimu maisha ya watu.
Kwa hiyo, limependekeza kuundwa kwa kamati maalumu ya kitaifa na
mkoa kwa ajili ya kuangalia suala hilo kwa undani zaidi ili kuondoa hofu
inayojengeka katika jamii dhidi ya Uislamu.
Wito huo ulitolewa jana na katibu mkuu wa Bakwata, Sheikh Suleiman
Lolila wakati akitoa salamu kwenye Baraza la Maulid lililofanyika
kitaifa wilayani Iramba, mkoani Singida.
Alisema miezi kadhaa iliyopita pamekuwepo na matukio ya kutisha
maeneo ya Mwanza, Mkuranga mkoani Pwani, Morogoro na Tanga ambayo
yamesababisha vifo vya Watanzania kadhaa wasio na hatia.
“Baraza Kuu la Waislamu Tanzania limesikitishwa sana na matukio hayo
ambayo yameleta vifo vingi. Baraza linasikitika sana Uislamu kuhusishwa
na ugaidi,” alisema Lolila.
Alibainisha kuwa suala linalowasikitisha zaidi Waislamu ni wahalifu
hao wa ugaidi mara nyingi kujitambulisha kuwa ni waumini wa dini ya
Kiislamu.
Alisisitiza kuwa Uislamu hauungi mkono vitendo hivyo vya ugaidi kwa
kuwa ugaidi ni haramu, hivyo ni lazima upigwe vita kwa namna yoyote ile.
Alisema Mtume Muhammad alihimiza amani, umoja na mshikamano baina
ya Waislamu wote ambapo alilinganisha umoja huo sawa na viungo vya
mwanadamu.
Aidha, Bakwata itaendelea kukariri wito wake wa kuwataka Waislamu
nchini kuondoa mafarakano baina yao na kuimarisha umoja, mshikamano na
mambo yote yenye maslahi kwao.
No comments:
Post a Comment