
WATU watatu
wanaosadikiwa kuwa ni majambazi wa kutumia silaha, ambao wamehusika kufanya
matukio mbalimbali ya kihalifu katika mkoa wa Dar es Salaam, wameuawa na
majambazi wenzao katika eneo la Vikindu wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani.
Licha ya
kuuawa kwa majambazi hao, Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam,
limefanikiwa kuwakamatwa watu zaidi ya saba, wanaosadikiwa kuhusika na tukio la
majibizano ya risasi na polisi, lililotokeo Vikindu lililosababisha kifo cha
askari mmoja.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Kamishna wa Polisi Kanda
Maalumu, Simon Sirro alisema kabla ya kuuawa watuhumiwa hao walikamatwa katika
maeneo tofauti ya Mbagala, Keko na Kawe jijini humo.
Alisema watu
hao walikamatwa kufuatia tukio la ujambazi, lililotokea Agosti 29, mwaka huu
katika Jengo la Sophia House maeneo ya Veta Changombe, ambapo majambazi hao
walidaiwa kupora Sh milioni 35 na kutoweka kwa kutumia gari aina ya Toyota Noah
lenye namba bandia T 549 BPK.
Aliongeza
kuwa uchunguzi wa tukio hilo, uliendelea kufanyika na Septemba 3, timu ya
upelelezi kutoka Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, iliweka mtego na kufanikiwa
kuwakamata majambazi hao watatu na walipohojiwa walikiri kufanya matukio
mbalimbali ya ujambazi wa kutumia silaha na kuweza kutaja silaha mbalimbali
walizonazo.
Kamanda
Sirro alisema majambazi hao, waliwapeleka askari eneo la Mbezi Chini katika
nyumba waliyokuwa wamekodi na askari walifanya upekuzi na walifanikiwa kupata
silaha mbalimbali, zikiwemo bunduki 23 na risasi zaidi ya 800 na vitu
vinginevyo.
Alitaja
silaha hizo kuwa ni bunduki za kijeshi tatu aina ya SMG zikiwa na magazini nane
na risasi 120, bastola 16, magazini tatu za bastola na risasi moja, Shot gun
pump action tatu na risasi 130, bastola 16 magazini na risasi 548 na bunduki
tatu aina ya Shot gun na risasi zake 130.
Aidha
alisema walikuta redio za mawasiliano 12 na chaja zake tatu, darubini za kuonea
mbali tatu, pingu za plastiki 45, majaketi ya kuzuia risasi matatu, mkasi mmoja
wa kukatia vyuma, mtarimbo mmoja, risasi baridi za kutishia 37, boksi moja la
kusafishia silaha, nyundo kubwa moja, pingu za chuma tatu, mashine moja ya
kuhifadhia kumbukumbu na magari mawili.

Alisema
uchunguzi wao ulibaini kuwa majambazi hao Septemba 6, mwaka huu walipora
bunduki aina ya Shot gun yenye namba 006091830, ikiwa na risasi moja katika
barabara ya Mbozi Chang’ombe.
Sambamaba na
hayo, majambazi hao walikiri kuhusika na wizi wa mamilioni ya fedha katika
Benki ya Habib African ya Kariakoo mwaka 2014 na Benki ya Stanbic mwaka 2014,
wakitumia gari aina ya Toyota Noah.
Kamanda
Sirro alisema baada ya mahojiano zaidi, majambazi hao walisema wanazo silaha
nyingine ambazo wamezificha Vikindu wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani. Ndipo
askari walifuatana na watuhumiwa hao hadi kwenye msitu wa Vikindu.
Alisema
askari walipofika eneo hilo, walilodai ni karibu na zilipo silaha hizo,
walishuka kwenye gari na kuingia porini wakiwa wamewatanguliza watuhumiwa mbele
majira ya usiku.
Aliongeza
kuwa wakiwa msituni humo na askari wakiwa wenye tahadhari kubwa, ghafla
walisikia milio ya risasi ikitokea mbele, ambapo askari walilala chini na
baadaye zikisikika sauti zikisema ‘mmetuua sisi’.
Alisema
baada ya risasi za mfululizo kutulia, askari walishuhudia majambazi hao ambao
walichelewa kulala chini wakati risasi zikipigwa wakiwa wamejeruhiwa sehemu za
kifuani na tumboni huku wakivuja damu nyingi.
Alisema
askari walipiga risasi kuelekeza eneo zilikotokea risasi na walipoendelea
kusonga mbele, walikuta silaha aina ya SMG ikiwa imetelekezwa na haikuwa na
risasi ndani ya magazine, hivyo kufanya idadi ya silaha za SMG kufikia nne.
Aidha
alisema askari waliwabeba majambazi hao na kuwapeleka kwenye gari kuelekea
hospitalini, lakini wote walifariki dunia wakiwa njiani kutokana na kutoka damu
nyingi.
Akizungumzia
tukio la Vikindu, Sirro alisema wamefanikiwa kuwakamata watu hao wanaosadikiwa
kuhusika na tukio ambalo lilisababisha kifo cha askari mmoja.
“Majambazi
hao walikuwa ni kundi la kama watu 14 na tayari tumewakamata zaidi ya saba
ambao mpaka sasa tunawashikilia kwa mahojiano zaidi ili kufanikisha upelelezi,”
alisema Kamanda Sirro.
Pia alisema
kumekuwa na taarifa mbalimbali, zikisambazwa katika vyombo vya habari zikidai
kuwa katika tukio la Vikindu, kuna askari anahusika na tukio hilo na kudai taarifa
hizo si za kweli na hakuna askari aliyehusika katika tukio hilo.
Katika tukio
lingine, jeshi hilo limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa wanne kwa makosa ya wizi
wa magari manane, likiwemo gari moja la kibalozi.
Kamanda
Sirro alisema magari hayo yaliibwa jijini Dar es Salaam na kuuzwa kwa watu
mbalimbali jijini hapo na mikoani na watuhumiwa wote wanaendelea kuhojiwa na
mara upelelezi utakapokamilika watapelekwa mahakamani kujibu tuhuma
zinazowakabili.
Sirro
alisema katika tukio lingine jeshi hilo limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa sita
wanaodaiwa kuhusika na kuvunja nyumba usiku na kuiba.
Alisema
watuhumiwa wote wanaendelea kuhojiwa na mara upelelezi utakapokamilika
watapelekwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.
No comments:
Post a Comment