MTU na mkewe
wamenusurika kifo, baada ya nyumba yao walimokuwa wamelala kuchomwa moto na
kuteketea yote.
Aliyeteketeza
nyumba hiyo ni mwanamume mmoja, akidhani kuwa mke wake waliyetengana miezi
kadhaa iliyopita amelala ndani ya nyumba hiyo, ili aweze kumuua.
Kamanda wa
Polisi mkoani Mara, Ramadhani Ng’anzi, alisema jana kuwa tukio hilo limetokea
usiku wa kuamkia juzi katika kitongoji cha Mlimani eneo la Balili kona, mjini
Bunda.
Alisema kuwa
wazee walionusurika kifo baada ya nyumba yao kuchomwa moto ni Malenya Maduhu
Suba (68) pamoja na mke Kabula (52), ambao wote ni wakazi wa kitongoji hicho.
Ng’anzi
alisema siku ya tukio mwanamume huyo aliambiwa na mama mkwe wake kuwa mke wake
waliyeachana naye miezi sita iliyopita na kuolewa na mwanamume mwingine yuko
nyumbani kwa wazee hao amekuja kuwasalimia hao wakwe zake, ambao kwa sasa
kijana wao ndiye amemuoa mwanamke huyo.
Baada ya
mwanamume huyo kupata taarifa hiyo usiku wa manane aliamka na kwenda hadi
nyumbani hapo na kisha kuichoma moto nyumba hiyo, akidhani kuwa mke wake ambaye
tayari wameshaachana naye pia amelala ndani ya nyumba hiyo.
Aidha,
alisema ndani ya nyumba hiyo kulikuwa na hao wazee wawili tu, kwani huyo
mwanamke alikuwa amelala katika mji mwingine. Alisema hao wazee walinusurika
baada ya kukimbilia nje, lakini wakiwa wamejeruhiwa na moto huo na kwamba kila
kitu kilichokuwa ndani ya nyumba hiyo zikiwemo samani zote za ndani pamoja na
kuku wakubwa 17 na vifaranga 18 vyote viliteketezwa na moto huo.
Mwenyekiti
wa kitongoji hicho, Francis Paul alisema wananchi walifanikiwa kumkamata
mtuhumiwa huyo Mathias Masalu (26) na kumpeleka polisi. Mzee ambaye nyumba yake
ilichomwa moto alisema kuwa thamani ya vitu vyote ni Sh milioni 2.5.
No comments:
Post a Comment