Naibu Spika
wa Bunge, Dk Tulia Ackson sasa amesababisha makubwa zaidi; wabunge kutoka vyama
vya upinzani wako radhi kutimuliwa wote iwapo kiongozi huyo ataongoza vikao
vyote vilivyosalia na wao kuendelea na msimamo wao wa kumsusia.
Jana, Dk
Ackson aliingia kuongoza kipindi cha maswali na majibu na wabunge wote wa vyama
vya upinzani wakatoka ndani ya ukumbi na alipomuachia mwenyekiti wa Bunge,
Andrew Chenge kuendelea na shughuli zilizosalia, walirejea ukumbini.
“Kama Naibu
Spika atakuwepo kwenye kile kiti, hatatuona bungeni, hata kama ni leo, ni kesho
hata Bunge lote. Tuko tayari kuchukua gharama hiyo,” alisema kiongozi wa Kambi
Rasmi ya Upinzani, Freeman Mbowe akiwa nje ya ukumbi wa Bunge baada ya kuongoza
wabunge wenzake kutoka ukumbini wakati wa kipindi cha maswali na majibu.
Kauli hiyo
ya Mbowe imekuja siku moja baada ya Dk Ackson kukataa Bunge kujadili sakata la
wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) waliotimuliwa kwa maelezo kuwa
hawafundishwi kwa muda mrefu kutokana na walimu wao kugoma wakidai malimbikizo
yao.
Kitendo cha
Dk Ackson kukataa hoja hiyo ijadiliwe, kilisababisha vurugu bungeni kiasi cha
kuita askari kuingia kuwatoa wabunge waliokuwa wakipiga kelele na baadaye
kuwaamuru waliokataa kukaa waondoke ukumbini.
Wakiwa nje,
walifikia uamuzi wa kususia vikao vyote vitakavyoongozwa na Naibu Spika na
wakaanza kutekeleza uamuzi huo jana asubuhi.
Kauli ya
Mbowe pia imekuja siku moja baada ya Kamati ya Maadili, Kinga na Haki za Bunge
kuwasimamisha wabunge saba kutoka vyama vya upinzani kuhudhuria vikao vya
kuanzia mkutano huu hadi ujao kwa maelezo kuwa walifanya fujo wakati wakipinga
hoja ya Serikali ya kusimamisha matangazo ya moja kwa moja ya baadhi ya
shughuli za Bunge.
Jana, Mbowe
alisema wako tayari kutimuliwa wote kama uamuzi huo utawapendeza viongozi wa
Bunge kwa kuwa siasa inaweza kufanywa ndani na nje ya Bunge.
Mbowe
alisema kuwa hali ilishafika hatua nzuri ya kujenga demokrasia nchini na kwamba
pamoja na matatizo yaliyokuwepo, hali ilikuwa ikienda vizuri.
“Lakini
tangu kuingia kwa Serikali ya Awamu ya Tano mnaweza kuona Bunge limegeuka
kituko. Bunge limegeuka mahali pa kukomoana. Bunge limekuwa mahali pa
kutishana,” alisema Mbowe.
“Naibu Spika
anaamua kusitisha mjadala wa maana ili apate muda wa kuwadhibiti na kuwafukuza
wabunge bungeni na anaona sifa.
Tunaacha
kujadili hoja ya msingi kama mambo ya Udom. Watoto wadogo wanalala nje haoni ni
muhimu, anaona muhimu ni kuwafukuza wabunge wa upinzani.”
Mbowe,
ambaye pia ni mbunge wa Hai, alisema hawezi kukaa, kumsikiliza na kumheshimu Dk
Ackson, bali wapinzani wataheshimu anayewaheshimu bila kujali anatoka chama
gani na hawatamuheshimu asiyewaheshimu bila kujali cheo chake.
“Sasa leo
(jana) tumekataa kushiriki kipindi cha maswali na majibu kwa sababu yeye (Dk
Ackson) anasimamia kipindi hicho na akitoka tutarudi bungeni.
Akija
mwenyekiti, akija Spika mwenyewe tutarudi bungeni. Lakini kama Naibu Spika
atakuwepo kwenye kile kiti hatatuona bungeni, hata kama ni leo, ni kesho hata
Bunge lote. Tuko tayari kuchukua gharama hiyo,” alisema Mbowe.
No comments:
Post a Comment