SERIKALI
imemsimamisha msambazaji wa mafuta Kampuni ya Sahara Energy Resourses Limited
ya Nigeria aliyeingiza mafuta ya ndege (JET A1) yaliyochafuka na kumtaka
kusafisha matangi pamoja na mabomba ya mafuta ya kampuni zilizopokea mafuta
hayo.
Aidha,
imeelezwa pamoja na kutokea kwa tatizo hilo la kuchafuka kwa mafuta hayo nchi
haitaingia katika ukosefu wa nishati hiyo muhimu kwa kuwa kuna akiba ya kutosha
kwa siku 14 na tayari kampuni ya Puma imeagiza mafuta ambayo yataingia nchini
Juni 7, mwaka huu.
Waziri wa
Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alitoa kauli hiyo jana wakati
alipotembea kampuni za mafuta zilizopokea mafuta yaliyochafuka kwa
kuchanganyika na petroli jijini Dar es Salaam ili kubaini ukweli wa uhaba wa
mafuta ya ndege.
Profesa
Muhongo aliiagiza kampuni hiyo ya Sahara Energy Resources Limited ya Nigeria
kuhakikisha inasafisha matangi pamoja na mabomba ya mafuta kuanzia leo na kama
haitatekeleza hilo itakuwa ni mwisho kufanya kazi nchini.
“Msafishe
haya matenki pamoja na mabomba yote kwa gharama zenu. Haya ni maagizo sisi
hatuwezi kuendelea kusubiri, hamuwezi mkasababisha nchi ikawa na uhaba wa
mafuta kwa majadiliano yenu ambayo hayana mwisho.
“Usafishaji
unatakiwa kuanza kesho, kama hautafanyika kuanzia hiyo kesho, basi Sahara
isahau kufanya biashara katika nchi hii. Na sio hilo tu hata tenda (zabuni)
alizokuwa amepata nazo tutazifuta,” alisema Profesa Muhongo.
Alisema kuwa
kampuni hiyo haitakiwi kupewa zabuni nyingine hadi hapo uchunguzi
utakapokamilika wa kubaini ukweli wa mafuta hayo kuchafuka kwa kuchanganyika na
petroli.
Profesa
Muhongo alisema hatua walizochukua ya kwanza ni kumsimamisha kujihusisha na
zabuni yoyote itakayotangazwa kuanzia sasa lakini pia kutakiwa kusafisha
matangi na mabomba hayo.
Aliongeza
kuwa hii ni mara ya pili kwa kampuni hiyo mafuta yake kuwa na tatizo kwani mara
ya kwanza mafuta yake yalibainika kuwa machafu akarudishwa nayo.
Awali
mwakilishi wa kampuni hiyo ambaye yuko hapa nchini alisema, hawana sehemu ya
kuhifadhi mafuta hayo ambayo yamechafuka hivyo wanasubiri meli yao irudi ili
waweze kuyaondoa mafuta.
Hata hivyo,
kampuni ya kuhifadhi mafuta nchini ya Tanzania International Petroleum Reserves
Limited (TIPER) ilimhakikishia Profesa Muhongo kuwa wana nafasi ya kuhifadhi
mafuta yote yaliyochafuka, hatua ambayo waziri huyo aliiagiza kampuni hiyo
kuhifadhi mafuta hayo katika matangi ya TIPER badala ya kusubiri meli.
“Hilo
linatuchelewesha TIPER wameshakubali wana nafasi ya kuhifadhi hayo mafuta, kwa
hiyo yahifadhi hapa ili msafishe hayo matenki, ili mafuta yatakayokuja yakute
matenki ni masafi,” alisema.
Aidha,
alisisitiza kuwa taifa haliwezi kuingia kwenye uhaba wa mafuta ya ndege na yapo
ya kutosha siku 14 kwani kampuni ya Puma tayari imeshaomba mafuta kutoka katika
kampuni za Total na SP ya Rwanda.
Pia meli ya
Puma itaingia nchini Juni 7 na meli nyingine itaingia Juni 13.
Awali
akizungumzia hali hiyo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Uagizaji Mafuta
kwa Pamoja, Michael Mjinja alisema, meli hiyo iliingia nchini Mei 5, mwaka huu
na mafuta hayo yalithibitishwa kuwa na ubora na Shirika la Viwango nchini
(TBS).
Alisema
baada ya mafuta hayo kushushwa ilibainika kuwa yamechafuliwa hatua iliyowafanya
kumuagiza aliyeleta mafuta hayo kuyaondoa.
Naye
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA)
Felix Ngamlagosi alisema, kwa sasa kuna mafuta ya kutosha kwa siku 14 lakini
kuna hatua nyingine zinazochukuliwa ili kuhakikisha hakuna uhaba wa mafuta
utakaotokea.
“Hayo yaliyochanganyika kuna hatua
zinazochukuliwa ikiwa ni pamoja na kuchukua sampuli za pamoja na sisi ni
wasimamizi ili kuhakikisha zinapelekwa maabara na kujua kitu gani kilitokea,”
alisema.
Profesa
Muhongo alizitembelea kampuni hizo ambazo ni Puma Energy, Gapco Tanzania Ltd,
Oilcom, ORXY Energies na TIPER. Meneja wa Huduma za Usafiri wa Anga wa Oilcom,
Haruna Magota alimwambia Waziri Muhongo kuwa, mafuta waliyopokea yalikuwa ni
lita milioni 8.8 na wao walikuwa na lita milioni 2.6, ambapo mafuta hayo yote
yameharibika.
Alisema
ukosefu wa mafuta hayo umekuwa ni tatizo kwa wateja wao ambao ni mashirika ya
ndege kwani jumla ya lita milioni 10.8 yote yamechafuka.
Aidha
aliongeza kuwa wakaguzi wa meli walishawahi kutoa onyo kwa kampuni hiyo kuwa
meli zake hazina viwango vinavyotakiwa vya kubeba nishati hiyo.
Aidha
kampuni za kuagiza mafuta nchini zilitaka kampuni ya Sahara Energy Resources
Ltd ya nchini Nigeria kuweka hadharani uthibitisho wa kuhujumiwa kuhusiana na
kashfa ya uingizaji mafuta ya ndege machafu hapa nchini inayolikabili shirika
hilo.
Kwa mujibu
wa taarifa ya Chama cha Waagizaji Wakubwa wa Mafuta ya Petroli nchini (TAOMAC)
iliyosambazwa kwenye vyombo vya habari jijini Dar es Salaam juzi, waagizaji hao
waliitaka kampuni hiyo kutaja jina la kampuni au mhusika yeyote anayeaminika
kuihujumu kampuni hiyo kama ambavyo imenukuliwa na vyombo vya habari nchini
ikijitetea kupinga kashfa hiyo.
“Tunawaomba
wenzetu hawa wahakikishe wanakabidhi jina la kampuni au mtu yeyote wanayemshuku
kuwa anahusika na kashfa inayowakabili kwa Jeshi la Polisi au chombo chochote
cha usalama nchini vinginevyo sisi tutaamini kuwa utetezi wao ni uwongo na
unalenga kutafuta njia ya kutokea,’’ alisema Mkurugenzi Mtendaji wa TAOMAC,
Salum Bisarara kupitia taarifa hiyo.
Sakata la
kuingizwa kwa mafuta machafu ya ndege aina ya Jet A1 na hofu ya kukosekana kwa
mafuta hayo nchini liliibuliwa na Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto
Kabwe wakati akichangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini kwa
mwaka wa fedha 2016/2017, alisema mafuta hayo yatakosekana kutokana na kampuni
moja ya kigeni iliyopewa zabuni kuagiza mafuta hayo, kuingiza mafuta ambayo
hayawezi kutumiwa na ndege.
No comments:
Post a Comment