
Mchungaji Donald Mwakisambwe wa kanisa la Kipendekoste la
Kiinjili Tanzania, kwenye ofisi za gazeti hili wakati akitoa ushuhuda wa
kufanya biashara haramu ya madawa ya kulevya.
Kinara wa kimataifa wa kuuza madawa ya kulevya aliyezunguka
sehemu mbalimbali duniani kuuza mihadarati, ameacha biashara hiyo na sasa
anahubiri Injili kupiga vita dawa hizo. Kigogo huyo Mtanzania na mzaliwa wa
Mbeya, ambaye sasa anajiita kiumbe kipya katika Kristo, ni Mchungaji Macdonald
Mwakisambwe wa Kanisa la Kipentekoste la Kiinjili jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na NIPASHE Jumamosi
jana, Mwakisambwe alisema alianza biashara ya unga mwaka 1990 na kuifanya kwa
miaka 10, akisafirisha dawa kwa maelfu ya wateja walioko Afrika, Asia, Ulaya na
Amerika. Alisema katika kutimiza azma hiyo, alitumia pasi za kusafiria za
mataifa mbalimbali zenye majina tofauti, zikimuonyesha kuwa ni raia wa
Msumbiji, Tanzania, Kenya, Namibia, Afrika Kusini na Namibia.
Alieleza kuwa, kumiliki pasi hizo kulilenga kuficha
wanausalama wasimgundue kuwa ni ‘mzungu wa unga’ aliyekuwa anasafiri nchi
mbalimbali duniani ndiyo maana kila alipomaliza mzunguko aliziharibu pasi hizo
. Alisema mwaka 1999, Yesu Kristo, alimtokea akiwa rumande kwenye gereza la
Industrial Area jijini Nairobi, baada ya kuwasili Kenya akitokea Karachi,
Pakistani akiwa na karibu kilo moja ya kete za heroin tumboni.
Mwakisambwe alisema alipotua Nairobi, alikamatwa na maofisa
wa polisi kadhaa waliomueleza kuwa ni muuza unga wa kimataifa na kuwekwa chini
ya ulinzi kwenye kizuizi cha Uwanja wa Ndege wa Jomo Kenyatta. “Nilikuwa na
pasi ya Msumbiji yenye jina la Danilo Silva Jalla, licha ya kwamba ni
Mtanzania”,anasema.
Anaongeza kusema kuwa ili kupata pasi hizo, alibadilishwa
sura halisi kwa kujiwekea ndevu za bandia, nyusi na nywele nyingi zilizompa
sura tofauti na muonekano mpya kila alipouhitaji. Alisema pasi hizo zilikuwa
zikitengenezwa na magenge ya wanaojihusisha na madawa hayo ambao wapo kila
mahali na wamewekwa mahsusi kufanikisha usambazaji wa mihadarati kila sehemu
inapohitajika.
Alisema hata hapa Tanzania, kuna magenge hayo ya ‘mafia’ na
mtandao huo unashirikiana na maofisa wa Idara ya Uhamiaji wasio waaminifu.
Mchungaji Mwakisambwe alisema kupitia biashara hiyo, alijenga nyumba kadhaa
zilizoko Dar es Salaam na Mbeya pia alikuwa na utajiri mkubwa wa magari ya
kifahari na mengine ya kutanulia.
Alieleza kwa kirefu jinsi dawa hizo zinavyomezwa na
kusafirishwa na kukanusha madai kuwa yanaingizwa tumboni kupitia njia ya haja
kubwa. Alisema yanamezwa kama vidonge vingine baada ya kufungwa ndani ya vifuko
ya nailoni, kisha kuzungushiwa gundi ya karatasi ya nailoni, kuzongwa na
vipande vya glovu nyepesi ambazo hufungwa kikamilifu na kuchomwa kwa moto kama
pipi kifua ili kuvidhibiti visifunguke na dawa kuyeyuka tumboni. “Kete
zinazomezwa zina ukubwa wa kidole gumba cha mtu mzima na hutofautiana kwa
uzito, zipo zenye gramu 10 na ndogo zina gramu tano.
Ukiwa mzoefu unaweza kumeza hata 100 na kubeba pipi zenye
uzito wa kilo moja. ”
Mchungaji huyo ambaye sasa anasema anachohitaji ni kuwaeleza
watu kuwa Mungu hapendi biashara ya madawa na kutangaza wokovu, na kusisitiza
kuwa aliyemuondoa kwenye biashara hiyo ni Yesu Kristo.
No comments:
Post a Comment