WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Mambo ya
Ndani ya Nchi kupitia Jeshi la Polisi kufanya upelelezi kuwabaini waliohusika
na mauaji ya watu saba ambao miili yao iliokotwa pembezoni mwa mto Ruvu
wilayani Bagamoyo, mkoa wa Pwani, ikiwa kwenye mifuko ya sandarusi, ili hatua
kali zichukuliwe dhidi yao.
Waziri Mkuu Majaliwa amesema serikali imepokea kwa huzuni
kubwa taarifa ya kuokotwa kwa miili hiyo Desemba 8, mwaka huu na kueleza kuwa
matukio kama hayo, likiwemo la mjasiriamali kuuawa baada ya kutekwa mkoani
Tabora, hayavumiliki wala kukubalika.
Alitoa maagizo hayo jana katika Baraza la Maulid ya kuzaliwa
Mtume Muhammad (S.A.W) lililofanyika kitaifa kijijini Shelui wilayani Iramba
mkoani Singida. Waziri Mkuu Majaliwa alikuwa mgeni rasmi.
Alisema, “Serikali kwa kushirikiana na Polisi, tena Waziri
wa Mambo ya Ndani uko hapa (akimzungumzia Mwigulu Nchemba aliyekuwepo katika
baraza hilo), tutaendelea na upelelezi ili wahusika wachukuliwe hatua kali.”
Jana akihojiwa katika kituo cha televisheni cha Star TV,
Mwigulu alisema uchunguzi umebaini kuwa miili saba iliyookotwa Bagamoyo ni ya
wahamiaji haramu.
Miili ya watu sita ilikutwa Desemba 7, mwaka huu kando ya
mto Ruvu wilayani Bagamoyo ndani ya mifuko ya sandarusi na ikiwa imewekwa mawe
ili isielee kisha mifuko hiyo kushonwa kama mzigo wa mazao na kutupwa mtoni.
Mwili mwingine uliokotwa Desemba 9, eneo hilo hilo na pamoja
na kutokuwa katika mfuko wa sarandusi, ulikuwa umevuliwa shati na kuonekana na
majeraha mgongoni na kwenye ubavu umekatwa na kitu chenye ncha kali.
Mwishoni mwa wiki, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani,
Boniventure Mushongi alisema miili yote ilizikwa kwa kuwa ilikuwa vigumu
kuwatambua kutokana na kuharibika vibaya huku kukiwa hakuna kitambulisho
chochote kinachoashiria watu hao ni nani na wametoka wapi na kwamba Polisi
inaendelea na upelelezi kubaini waliohusika na mauaji hayo na atakayebainika
sheria itachukua mkondo wake.
Aidha, Waziri Mkuu alisema serikali ipo macho kukabiliana na
tishio lolote la usalama na vyombo vya usalama vipo tayari muda na wakati wote.
Aliwataka wananchi kushirikiana na vyombo vya usalama kutoa
taarifa wanapoona kuna hatari kwani viongozi wa dini na waumini wa dini hizo
ndio walinzi wa Taifa.
Alisema uwepo wa vikundi vya uhalifu kama ‘panya road’ cha
jijini Dar es Salaam ni hatari kwa jamii, kwani vinadhuru na kuvuruga amani na
kueleza kuwa ni vijana na watoto wanaoishi katika jamii, walioko misikitini na
makanisani na kutaka waripotiwe katika vyombo vya usalama ili washughulikiwe.
Alizungumzia ugaidi na kubambikizwa kesi, na kusema serikali
itaendelea kusimamia mtu kupata haki zake na anayestahili adhabu, kuipata vile
vile.
“Ni heri kuwa na watu 10 waliotoroka mahabusu kuliko mtu
mmoja kukaa mahabusu kwa kesi ya kuonewa,” alisema Majaliwa.
Mwigulu anena kuhusu miili 7, Saanane
Akizungumza jana kwa simu kuhusu vifo hivyo vya Bagamoyo,
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba alisema serikali baada ya
tukio hilo ilichukua hatua kupitia vyombo vya usalama na tayari Mkuu wa Jeshi
la Polisi nchini, Inspekta Jenerali, Ernest Mangu amemhakikishia wanalifanyia
kazi.
“Kama nilivyosema awali, hatujajua asilimia mia kwa mia kama
watu hao waliouawa wana connection (uhusiano) na wahamiaji haramu waliookotwa
wamechoka sana hivi karibuni (juzi).
“Kuna wahamiaji 81 waliokotwa hawajitambui, wameishiwa nguvu
kabisa, ni eneo hilo hilo kulikookotwa miili hiyo, tumehisi watu waliowabeba
wahamiaji hao inawezekana wengine walikufa na kwa vile hawana utu, wakawafunga
katika viroba (sarandusi) na kuwatupa, Polisi wanachunguza hili kwa kina,”
alieleza Mwigulu.
Aidha, alisema pia Polisi inachunguza ikiwa miili hiyo
ilitupwa kikatili na wasafirishaji wa binadamu ambao nao hawana utu.
Alipoulizwa kwa nini wazikwe haraka bila vipimo vya
vinasaba, Mwigulu alisema kuwa alizungumza na IGP na kuelezwa kuwa miili hiyo
ilikuwa katika hali mbaya sana, lakini pia kuzikwa hakuzuii uchunguzi kufanyika
kujua chanzo cha vifo hivyo.
Kuhusu kupotea katika mazingira ya kutatanisha Ofisa wa
Ofisi ya Chadema, Makao Makuu Dar es Salaam, Bernard Saanane Novemba 18, mwaka
huu, Mwigulu alisema aliona taarifa hizo kupitia mitandao ya kijamii na kwa
kuwa alikuwa akimfahamu, alimpigia simu na kubaini simu haipatikani.
“Nilishtuka kuona hizi habari, binafsi ni rafiki yangu wa
karibu, nilipoona hizi habari nilimpigia na sikumpata, baada ya kuona simpati
nilimpigia Mbowe (Freeman- Mwenyekiti wa Chadema Taifa), lakini simu yake
iliita kama vile mtu yupo nje ya nchi,” alifafanua Mwigulu.
Hata hivyo, alisema amemuagiza IGP awaagize polisi kumtafuta
Saanane na kuhakikisha ufumbuzi wa kupotea kwake unapatikana na kujulikana
alipo.
Juzi, Mwenyekiti wa Umoja wa Kizazi cha Kuhoji Tanzania
(UTG), Malisa Godlisten akizungumza na waandishi wa habari, aliipa Chadema na
taasisi za umma zenye dhamana ya usalama wa raia saa 72 kuanzia jana
kuhakikisha Saanane anapatikana na kueleza umma chanzo cha vifo vya watu hao
saba ambao miili yao ilikutwa kando ya mto Ruvu, Bagamoyo.
No comments:
Post a Comment