
WAZIRI wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa
Joyce Ndalichako, ametoa masharti mapya ya ajira za ualimu nchini, huku akisema
Serikali haitaajiri walimu wa masomo ya sanaa (arts) kwa kuwa wapo wa kutosha.
Akizungumza mjini Dodoma jana wakati akifungua mkutano mkuu
wa mwaka wa Wakuu wa Shule za Sekondari Tanzania (TAHOSSA), Profesa Ndalichako,
alisema Serikali kwa sasa haiwezi kuajiri walimu wa masomo hayo kwa kuwa
inataka kuajiri walimu wa masomo ya sayansi na hisabati ambao idadi yao ni
ndogo.
“Pamoja na uamuzi huo mpya, ajira za walimu wapya wa masomo
ya sayansi nazo zimebadilika kwani wale wote waliohitimu ualimu wa sayansi na
hisabati, wanatakiwa watume vyeti vyao kabla ya kupangiwa kituo cha kazi.
“Kuhusu wale walimu wa ‘arts’, kule tuna walimu wa ziada
ambao tutajaribu kuwapanga kutokana na shule, kwani wengi walikuwa wamepangwa
shule moja. Kwahiyo, tutaangalia utaratibu wa kuwapanga kulingana na
mahitaji,’’ alisema Profesa Ndalichako.
Akizungumzia suala la ubora wa elimu nchini, Profesa
Ndalichako aliwataka walimu wakuu hao kuhakikisha wanasimamia ubora wa elimu
kwa kuwa wao ndio wanaowaandaa wanafunzi kabla hawajaenda vyuoni.
“Vilevile pelekeni takwimu sahihi za wanafunzi waliopo
katika shule zenu kuisaidia Serikali katika kupanga bajeti ili iweze kutoa
fedha sahihi.
“Hapa kuna kimbembe, yaani wakati mwingine huwa najifanya
nimepoteza takwimu ya shule fulani, nikiziomba na kutumiwa, zinakuwa ni tofauti
na zile za mwanzo.
“Hili nawaomba mkalisimamie ili iwe rahisi kwetu kupanga
bajeti yenye tija,’’ alisema.
Kuhusu ujenzi wa maabara katika shule za sekondari, waziri
huyo alisema kwamba kutokana na nyingi kukamilika, Serikali itatoa vifaa vya
maabara kuanzia Januari mwakani baada ya kuwa vimeingia nchini kutoka
vilikoagizwa.
Awali, akisoma risala ya walimu hao, Rais wa TAHOSSA, Bonus
Nyimbo, aliiomba Serikali itoe waraka wa kupiga marufuku matumizi ya simu kwa
wanafunzi shuleni kwa kuwa zimekuwa zikichangia kushuka kwa ufaulu kwa baadhi
ya wanafunzi.
“Ili kuboresha elimu, tunaiomba Serikali itoe waraka wa
kupiga marufuku matumizi ya simu kwa wanafunzi kwani simu nyingi tunazozikamata
tunakuta mule hakuna taaluma,’’ alisema Nyimbo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Global Education Link,
Abdulmalik Molel, ambaye pia kampuni yake ilipewa tuzo ya heshima katika
kuendeleza elimu nchini, alisema ni jukumu la kila mmoja kutimiza wajibu wake
ili kuiendeleza elimu ya Tanzania.

“Kila mmoja anapaswa kutimiza wajibu, wazazi, walezi na
walimu, waambieni wanafunzi wasiwe na ‘expectation’ (matarajio) makubwa kwani
wanapokuwa na matarajio hayo, wakienda vyuo vikuu wanakuwa wasumbufu,” alisema.
Wakati hayo yakiendelea, juzi taarifa ilitolewa jijini Dar
es Salaam na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi,
Maimuna Tarishi, ikisema kwamba, walimu wahitimu wa masomo ya sayansi na
hisabati waliohitimu shahada na astashahada mwaka 2015, wanatakiwa kuwasilisha
nakala za vyeti vya elimu ya sekondari vya kidato cha nne na sita na taaluma ya
ualimu kwa uhakiki.
Pamoja na hayo, hivi karibuni Serikali ilitangaza kusitisha
ajira zote nchini ili kukabiliana na wimbi la watumishi hewa.
Sambamba na uamuzi huo, nyongeza za mishahara kwa watumishi
wa Serikali nazo zilisimamishwa ili kukabiliana na watumishi hao hewa ambao
walikuwa wakiingizia hasara Serikali.
No comments:
Post a Comment